Habari za Kitaifa

Shule zatarajia hali ngumu Serikali ikichelewesha mgao

Na  SAMWEL OWINO January 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WALIMU wakuu watakuwa na wakati mgumu baada ya wizara ya Fedha kusema itachelewa kutuma Sh48 bilioni za kufadhili elimu baadaye mwezi huu.

Wizara imezitaka shule ziwe na subira huku serikali ikifanya juhudi kuhakikisha kuwa masomo yanaendelea ifaavyo shuleni. Hii ni licha ya serikali kuruhusu shule zifunguliwe wiki hii licha ya walimu kulalamikia uhaba wa pesa.

Waziri wa Fedha, Bw John Mbadi alisema serikali inashirikiana kwa karibu na wizara ya Elimu ili kuhakikisha pesa zinaingia kwenye akaunti za shule kabla ya mwisho wa mwezi huu.

“Tunafanya kazi kwa karibu na wizara ya elimu ili kuhakikisha pesa zinatolewa kwa shule kwa wakati ili kuhakikisha masomo yanaendelea bila kukwama,” Bw Mbadi aliambia Taifa Leo.

Bw Mbadi alisema anafahamu wasiwasi ulioibuliwa na shule kuhusu kucheleweshwa kwa pesa lakini akawataka walimu wakuu wavumilie serikali kwa muda mfupi.

Alisema kuwa miezi ya Januari na Februari kwa kawaida ni miezi migumu sana kwa serikali lakini akashikilia kuwa elimu ni miongoni mwa wizara iliyopewa kipaumbele na Hazina ya Kitaifa.

“Tunachopatia kipaumbele mwaka huu ni kulipa mikopo, kutoa pesa kwa shule, mishahara na kutolewa kwa mgao wa Desemba kwa serikali za kaunti,” Bw Mbadi alisema.

Bw Mbadi alizitaka shule kuendelea na muhula huu wa kwanza akiwahakikishia kuwa hakuna shughuli zitakazositishwa kwa sababu ya ukosefu wa fedha.

“Shule zisifanye masuala ya fedha kuwa ya dharura, masomo bado yanaweza kuendelea hata kama hatujatoa fedha. Hata hivyo, nawahakikishia kuwa mishahara ya wafanyikazi wote wa shule italipwa,” Bw Mbadi alisema.

Waziri alidokeza kuwa katika tukio hilo, serikali haitaweza kupata Sh48 bilioni kwa awamu moja, ila itapata angalau nusu ya pesa hizo ambazo zitatolewa shuleni kabla ya mwisho wa mwezi huu.

Haya yanajiri huku baadhi ya wanafunzi wa Gredi ya 9 wakikumbwa na matatizo kadhaa ikiwemo ukosefu wa madarasa ya kutosha na vitabu.

Waziri wa Elimu, Bw Julius Ogamba katika taarifa iliyotolewa wiki jana, alizihakikishia shule kuwa wizara hiyo inashirikiana na Hazina ya Kitaifa kuhakikisha Sh48.38 bilioni zinatolewa.

Kiasi hicho ni pamoja na Sh4.12 bilioni kwa elimu ya msingi bila malipo, Sh15.32 bilioni kwa elimu ya shule za kutwa.

Haya yanajiri huku kukiwa na wito wa wabunge kuongeza ufadhili wa wanafunzi katika shule za msingi na za kutwa.

Wizara ya elimu inatarajiwa kujibu kauli iliyoombwa na Mbunge wa Suna Magharibi, Bw Peter Masara kuhusu kupungua kwa mgao wa pesa shuleni licha ya gharama ya maisha kuongezeka.

Bw Masara alisema ufadhili wa sasa unaotolewa na serikali kwa shule hauwezi kuzisaidia kuendelea huku akidai hii inaathiri ubora wa elimu kwani walimu wakuu wanalazimika kubuni mbinu za kukabiliana na upungufu huo.

IMETAFSIRIWA NA WINNIE ONYANDO