Habari za Kitaifa

Si mbolea feki tu, dawa za kupulizia mimea pia zimepatikana kuwa na sumu

April 6th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA FRANCIS MUREITHI

HUKU serikali ikikiri kwamba wakulima waliuziwa mbolea ghushi mwezi jana, uchunguzi mpya unaonyesha kuwa wanakodolea macho hasara zaidi kutokana na matumizi ya dawa zenye madhara.

Uchunguzi uliochapishwa katika jarida la kimataifa la EU Observer kwenye ripoti, Poison For Sale – The Pesticides Banned in EU in use in Kenya unafichua kuwa wakulima wa Kenya bado wanatumia dawa zilizopigwa marufuku kunyunyuzia mazao mashambani.

Kulingana na uchunguzi huo, dawa hizo zina kemikali yenye sumu aina ya Imidacloprid ambayo huangamiza nyuki.

Mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya kusaga pareto nchini (PPCK), V Justus Monda sasa ametoa mwito wa dharura kwa Serikali kuongeza msaada wa kifedha ili kufufua sekta ya pareto ambayo inazidi kufifia.

Aidha, amesema hii itawezesha wakulima kuongeza zao hilo ambalo hutengeneza dawa za kuangamiza wadudu mashambani ambazo hazina kemikali zenye sumu.

“Zao la pareto lina kiwango kidogocha sumu na limetumiwa kwa karne nyingi kama dawa mwafaka kumaliza wadudu sugu wanaoharibu mazao kote duniani,” akasema Bw Monda.

Alifafanua kuwa zao la pareto ni la kiasili ambalo ni salama kutumiwa mashambani na nyumbani kwani halina madhara kwa binadamu.

Alidokeza kuwa wakulima wenye mashamba madogo wanaokuza zao hili katika kaunti 19 kote nchini, wako tayari kuongeza ekari zaidi za pareto ili kuhakikisha Kenya inatoa kwa wingi zao hili na kuhakikisha kiwanda cha kusaga pareto kilichoko jijini Nakuru kinafanya kazi kwa muda wa saa 24.

Kwa sasa kiwanda cha PPCK jijini Nakuru husaga pareto iliyokauka angalau mara mbili kwa mwezi kutokana na upungufu wa zao hilo.

“Hii kasoro ya kiwanda cha PPCK kusubiri maua yaliyokauka kwa muda mrefu inaumiza wakulima na ndiposa natoa mwito kwa serikali kuu kuunga mkono kwa dhati kufufuliwa kwa kiwanda hiki ili wakulima waweze kuongeza uzalishaji wa pareto,” akasema Bw Monda.

Uchunguzi huo unatoa tahadhari kuwa baadhi ya dawa zinazoingizwa nchini kinyume cha sheria huenda zikawa na madhara mengi siku za usoni.