Sichoki: Raila azindua mpango wa mazungumzo ya kitaifa unaoendeshwa na wananchi
KIONGOZI wa ODM, Bw Raila Odinga, ameanzisha mpango kabambe wa mazungumzo ya kitaifa yanayoongozwa na wananchi, akisema utasaidia Kenya kukabiliana na changamoto zinazokua za kijamii na kisiasa, na kuanzisha upya utamaduni wa utawala bora.
Mpango huo, unaoitwa “Mkutano wa Kitaifa wa Kizazi kwa Kizazi”, unalenga kuwa jukwaa la mchakato wa chini kwenda juu ambapo wananchi kutoka kila kona ya nchi watakutana kujadili masuala muhimu na kutoa mapendekezo, yakihitimishwa kwa mkutano wa kitaifa utakaojumuisha wajumbe wa mashinani, wabunge, mashirika ya kijamii, na wadau wengine.
Katika mahojiano maalum na NTV na Taifa Leo nyumbani kwake Karen, Nairobi, Jumamosi, Bw Odinga alisema mpango huo unategemea Kifungu cha 1 cha Katiba ya Kenya, kinachosema mamlaka ya juu kabisa ni ya wananchi, na yanaweza kutekelezwa moja kwa moja au kupitia kwa wawakilishi waliochaguliwa.
“Sehemu ya wawakilishi waliochaguliwa inaeleweka — hiyo ni kuhusu uchaguzi. Lakini Wakenya milioni 55 watatumiaje mamlaka yao moja kwa moja? Hapo ndipo mazungumzo yanahitajika. Hiki ndicho kiini cha ‘sisi wananchi,’” alisema Raila.
Katika pendekezo lake, mazungumzo yataanzia ngazi ya kituo cha kupigia kura, ambapo wananchi wa makundi mbalimbali — vijana, wanawake, wazee, na watu wenye ulemavu — watakutana kujadili matatizo ya maeneo yao.
Bw Odinga anapendekeza vikundi vya watu 40 au 50 kwa ngazi ya chini kabisa, nusu yao wakiwa vijana wa kizazi cha Gen Z.
“Mikutano hiyo itachagua wawakilishi watakaowasilisha hoja kwa ngazi ya wadi, kisha kaunti ndogo, halafu kaunti, na mwishowe mkutano wa kitaifa.”
Katika kila hatua, wajumbe watatambua masuala muhimu na kuwachagua wawakilishi watakaowasilisha hoja katika ngazi inayofuata. Wakati mkutano wa kitaifa utakapofanyika, Bw Odinga anatarajia zaidi ya wajumbe 3,000 wakiwakilisha kaunti zote, wabunge, viongozi wa dini, vyama vya wafanyakazi, wasomi, mashirika ya kijamii, miongoni mwa wengine.
“Huu utakuwa mkutano wa kweli wa wananchi — si mkutano wa siasa. Na lazima uwe mkubwa kuliko ule wa NADCO. Ile ilikuwa mijadala ya tabaka la juu tu. Huu unaleta masuala ya mashinani hadi meza ya kitaifa,” alisema.
Bw Odinga alisisitiza kuwa mchakato huu hautategemea ufadhili wa serikali.
Badala yake, alisema lazima uwe harakati ya jamii inayojitegemea, ambapo wananchi watafadhili ushiriki wao katika ngazi ya mashinani.
“Mara tu unapoleta fedha na serikali, mchakato unapoteza uhalali wake. Huu si wakati wa posho. Watu wanakuja kuzungumza kuhusu matatizo yao — si kupata marupurupu,” alisema.
Alipoulizwa ni lini viongozi wa kitaifa kama Rais William Ruto au yeye mwenyewe watashiriki, Raila alisisitiza kuwa mkutano huo haukuanzishwa kwa ajili ya wanasiasa.
“Hata mimi si lazima nihusike isipokuwa nianze mashinani. Rais Ruto naye anaweza kuja kama mtu binafsi. Huu si mkutano wa Raila au Ruto — huu ni mchakato wa wananchi wa Kenya,” alieleza.
Ingawa alitetea haki ya kudai mabadiliko, Bw Odinga alionya kuwa wito wa kumuondoa rais pekee hautoshi kutatua matatizo ya Kenya.
“Ruto anaweza kuondoka na Gachagua achukue nafasi yake. Je, kuna tofauti gani? Lazima tuunde utamaduni wa uchaguzi wa haki, serikali inayofanya kazi, na kampeni zenye mipaka,” alisema, akisisitiza kuwa mabadiliko ya kikatiba ni suluhisho la muda mrefu kuliko kubadilisha utawala.
Alisema mapendekezo ya mkutano wa kitaifa yanaweza kupelekwa kwenye kura ya maamuzi kulingana na uzito wake.
“Mkutano huu ukishatoa maoni, hatua inayofuata ni utekelezaji. Hiyo inaweza kujumuisha mabadiliko ya Katiba — na hapo ndipo kura ya maamuzi itahitajika. Wakati huu, itakuwa kweli imeongozwa na wananchi, si kama BBI,” alisema akirejelea mchakato wa BBI alioufanya pamoja na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kabla ya uchaguzi wa 2022.
Kwa wale wanaodai kuwa upinzani umechoka na kauli za “mazungumzo,” Raila alisema hali ya sasa nchini inahitaji ushirikiano wa pamoja badala ya uasi au kukata tamaa.
“Tulipigania demokrasia ya vyama vingi kupitia maandamano, kifungo na kujitolea. Lakini pia tulijua wakati wa kuketi mezani. Mgogoro wa sasa ni kama ule. Tusipoketi kuzungumza, mbadala wake ni vurugu. Mimi nitakuwa daima balozi wa mazungumzo wakati ufaao.”