Habari za Kitaifa

Sifuna kikaangoni ODM ikikutana leo huku Oburu akisema hamtaki chamani

Na CECIL ODONGO July 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna leo anatarajiwa kukumbana uso kwa uso na wakosoaji wake ndani ya ODM wakati wa mkutano utakaoandaliwa jijini Nairobi huku chama hicho kikiendelea kukabiliwa na mgawanyiko kuhusu ushirikiano wake na utawala wa Rais William Ruto.

Kikao hicho kitaongozwa na kinara wa ODM Raila Odinga ambaye anatarajiwa kutoa dira ya chama huku baadhi ya viongozi wakitaka Bw Sifuna afurushwe.

Seneta Sifuna ambaye pia ni katibu mkuu wa ODM, aliwasha moto Jumanne iliyopita kutokana na mahojiano aliyofana katika runinga ya Citizen ambapo alidai mkataba kati ya ODM na UDA umekatika wala hautekelezeki.

Pia alimrukia Rais Ruto akisema kung’olewa kwake afisini ni jambo linalochukuliwa kwa umuhimu wa kitaifa.

“Kupitia orodha yangu, kumwondoa Rais Ruto madarakani ni jambo linaloongoza. Akitumwa seneti, nitamtimua afisini bila kupepesa jicho,’’ akasema seneta huyo na kuzua makabiliano makali na wanzake wa ODM ambao wamekuwa wakiimba wimbo wa ‘Tutam’.

Tangu mahojiano hayo, mpasuko ndani ya ODM umejitokeza huku viongozi wanaomuunga Bw Sifuna wakimtetea nao wale wanaompinga wakidai anatumiwa na upinzani kuyumbisha chama hicho kongwe nchini.

Ni kutokana na mgawanyiko huo ndipo Bw Odinga ambaye alimtetea Bw Sifuna wikendi akiwa Kakamega, alisema kuwa kutakuwa na mkutano wa kuzima maasi ili chama hicho ‘kiongee kwa sauti moja’.

Baada ya kumtetea Bw Sifuna mnamo Ijumaa Kakamega, mnamo Jumapili, Bw Raila alionekana kubadili wimbo akiwa eneobunge la Karachuonyo, Homa Bay akisema alinukuliwa vibaya na vyombo vya habari.

“Nilisema Sifuna ana haki ya kutoa maoni yake binafsi na wanachama wengi si lazima wafuate msimamo wake. Nilisema tutaketi kama chama na kujadili suala hili kisha tuibuke na msimamo wa chama,” akasema Bw Odinga.

“Maoni ya Sifuna yalikuwa yake kibinafsi na yale ya ODM yatatolewa baada ya mazungumzo ndani ya chama,” akasema Bw Odinga.

Jana, wakati wa mahojiano na kituo kimoja cha redio, Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga alisema wamemchoka Sifuna na anastahili kuondoka ODM badala ya kupiga vita vya ndani kwa ndani.

“Raila alisema Kakamega kuwa Sifuna ana haki yake, hata mimi nina haki yangu na kushirikiana kwetu kikazi na serikali ni uamuzi wa ODM wala si mtu mmoja.

“Hatuwezi kuwa na katibu mkuu wa chama ambaye anajiona, amejawa kiburi na mimi siwezi kukubali au kufuata kauli yake. Kama anajiona bora, basi ashauriane na Ababu Namwamba ili afahamu kilichomfika. Sifuna aondoke ODM,” akasema Dkt Oginga huku akishangiliwa na vijana.

Dkt Oginga alisisitiza kuwa mkutano wa leo lazima utoe mwelekeo thabiti wa chama kuhusu ushirikiano wake na UDA, akisema lengo la Bw Sifuna ni kuwarejesha katika siasa za maandamano.

“ODM inapita sifa zake (Sifuna) kama mwanasiasa na kama ana ujasiri ajiondoe tuone atabaki na nini bila umaarufu wa chama. Sasa amevuka mipaka na lazima tusimame imara kuwaambia wapinzani wetu ukweli,” akasema Dkt Oginga.

Suala la Bw Sifuna limeonekana kuwagawanya viongozi wa ODM kutoka Nyanza na wenzao wa Magharibi.

Duru zimearifu Taifa Leo kuwa wandani wa Bw Odinga kutoka Nyanza wanapanga kutumia mkutano wa leo kumkabili Bw Raila kutokana na mwenendo wake wa kuendelea kumtetea katibu huyo wa ODM, hali inayofanya wadhihakiwe nyumbani.

Viongozi wengine wa ODM ambao wamemshutumu Bw Sifuna ni Mbunge wa Makadara George Aladwa na mwenzake wa Alego Usonga, Samuel Atandi.

Kwa mujibu wa mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa, Javas Bigambo, kwa sasa uwezekano wa kumng’oa Bw Sifuna uko chini ila suala kuu litakuwa kudhibiti maoni kinzani yanayozua mgawanyiko. Anasema huu utakuwa mwanzo wa kumzima Bw Sifuna.

“Sidhani atabanduliwa ila hisia kali zitahanikiza,” akasema Bw Bigambo.

Itataka iafikie msimamo kuwa sauti yake kuhusu masuala mbalimbali itakuwa ikitoka kwa chama chenyewe. Hii itakuwa mwanzo wa kumkata Sifuna miguu kisiasa na kuzima uhuru ambao amekuwa akitumia kuzungumzia masuala ya uhusiano wa ODM na serikali,” akasema.

“Pia Bw Sifuna anastahili kufahamu kuwa umuhimu anaopata kwa sasa ni kwa sababu ni katibu wa ODM. Akizuiwa kuendelea kutoa matamshi hayo, basi itabidi achunge maneno yake kwa sababu maoni yake ya kibinafsi yatakuwa yanazimishwa,” akaongeza.