Siku Raila alipojiapisha kuwa ‘Rais wa Wananchi’ baada ya kubwagwa uchaguzini
MNAMO Januari 30, 2018, Kenya ilishuhudia mojawapo ya matukio ya kishujaa na ya kujitolea zaidi kwenye siasa zake, pale Raila Odinga, akiwa kiongozi wa upinzani aliyegombea urais mara ya nne, alipoamua kujiapisha kuwa “Rais wa Wananchi” katika Uhuru Park, Nairobi.
Uamuzi wa kujiapisha mbele ya maelfu ya wafuasi wake, ilikuwa si tu ishara ya mapambano, bali kilio cha haki. Uliakisi hali ya mioyo ya wananchi ambao walihisi kunyang’anywa sauti waliyotoa kupitia uchaguzi.
Hatua za kuelekea tukio hilo zilianza miezi kadhaa kabla, kupitia uchaguzi wa urais wa 2017 uliobishaniwa.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilitangaza Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi wa Agosti, lakini Muungano wa NASA ulioongozwa na Raila Odinga ulipinga matokeo hayo kwa madai ya kasoro nyingi katika uwasilishaji na ujumlishaji wa matokeo.
Katika hatua isiyokuwa ya kawaida, Mahakama ya Juu ilifuta uchaguzi huo ikiwa ni mara ya kwanza barani Afrika mahakama kufuta matokeo ya rais.
Katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Oktoba, Bw Odinga alikataa kushiriki, akisema IEBC haikuwa imefanya mabadiliko yoyote na hivyo haingeaminika kusimamia uchaguzi huru.
Baada ya hayo, nchi iligawanyika kati ya wale waliotaka uchaguzi mpya na wengine waliopendelea hali ya kawaida.
Bw Odinga aliamua kutumia ghadhabu hiyo na hali ya wananchi kupoteza imani, kutekeleza tukio la ishara la upinzani la kula kiapo ambacho, kwa maneno yake, “kingerudisha haki ya wananchi.”
Serikali ilitoa onyo haraka kwamba hatua hiyo ingechukuliwa kuwa uhaini, kosa lenye adhabu kali kulingana na sheria ya Kenya.
Bw Odinga alifika Uhuru Park akiwa amejiandaa kwa tukio hilo. Maelfu ya wafuasi walikuwa tayari wameshika bendera na hakukuwa na polisi wala onyo la serikali kuwapinga. Vyombo vya habari vilizuiwa kupeperusha matangazo ya moja kwa moja kwa amri ya serikali.
Saa nane na dakika arobaini na tano alasiri, Bw Odinga alionekana jukwaani akiwa amevaa shati nyeupe na kofia nyeusi, mkono wake wa kulia akiwa ameshika Biblia.
Kando yake alikuwa Mbunge wa Ruaraka T.J. Kajwang’, aliyekuwa amevaa joho la mwanasheria kuongoza kiapo, pamoja na wakili Miguna Miguna, ambaye alisaidia kufanikisha hafla hiyo fupi.
“Mimi, Raila Amolo Odinga, naapa kwamba nitaipigania taifa hili kama Rais wa Wananchi, na Mungu nisaidie.” Kwa wafuasi wake wengi, halikuwa tukio la kuonyesha tu, lilikuwa tamko la heshima, kuirejesha sauti ya wananchi waliopoteza imani katika uchaguzi uliodaiwa kuibwa.