Habari za Kitaifa

Sitawaomba msamaha na nitaendelea kuchanga makanisani, Ruto aambia maaskofu

Na  VITALIS KIMUTAI November 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto Jumapili alisisitiza kwamba ataendelea kuchangia maendeleo ya kanisa nchini licha ya lawama kutoka kwa Maaskofu wa Kanisa Katoliki.

Dkt Ruto, ambaye alihudhuria ibada ya kanisa huko Kericho, alisema kuwa kwa miongo mitatu iliyopita, amekuwa akichangia maendeleo ya kanisa na hawezi kuomba msamaha kwa kufanya hivyo.

“Hatuombi msamaha tunapomtolea Mungu kama vile Mungu alikuwa wa kwanza kutoa. Alitupa mwanawe (Yesu) na tutaendelea kutoa ili neno (la Mungu) liweze kuwafikia wengine,” Rais Ruto alisema.

Miaka 30

“Nimechanga fedha katika ujenzi wa makanisa katika miaka 30 iliyopita na sijawahi kukosa chochote. Mimi ni zao la kutoa. Tutaendelea kutoa mchango wetu na kujenga makanisa,” akaongeza Rais Ruto.

Kiongozi wa nchi alisema: “Kanisa na Serikali ni washirika katika kuhudumia watu wa Kenya. Tutaendelea kushirikiana na viongozi wa kidini na waumini katika maendeleo ya kanisa na nchi kwa manufaa ya watu.”

Akizungumza wakati wa maombi ya madhehebu mbalimbali, yaliyofanyika katika kituo cha Kipsitet eneo bunge la Soi Sigowet kaunti ya Kericho jana, Dkt Ruto alibainisha kuwa baadhi ya watu wanatoa rasilimali zao kwa kanisa ili kushindana na wengine na kwamba hiyo ni sawa maadamu injili inaenea.

“Tutatoa kwa ujenzi wa kanisa na kwa kazi ya Mungu. Sisi ni zao la utoaji. Ni Mungu aliyetoa kwanza ndiyo maana tuna bahati ya kutoa ili kueneza injili,” alisema Ruto.

Rais alizungumza huku kukiwa na msukosuko kutoka kwa Maaskofu wa Kikatoliki uliopelekea kurejeshwa kwa Sh2.8 milioni alizochanga akiwa na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja Jumapili iliyopita katika kanisa katoliki jijini Nairobi.

Askofu Mkuu wa Nairobi Anyolo

Askofu Mkuu wa dayosisi ya Kanisa Katoliki Nairobi, Philip Anyolo, alikataa pesa zilizochangwa kwa kanisa katoliki la Kayole-Soweto na Dkt Ruto na Bw Sakaja walipohudhuria ibada. Rais Ruto alitoa Sh2 milioni kwa ujenzi wa nyumba ya padre msimamizi wa parokia na Sh 600,000 kwa kwaya ya kanisa hilo Soweto huku Gavana Sakaja akitoa Sh200,000 – ambazo zote zilikataliwa.

Hayo yalijiri saa chache baada ya Baraza la Maaskofu wa Kenya kushambulia vikali serikali ya Dk Ruto kwa kuendeleza ‘utamaduni wa uwongo, kuwabebesha raia mzigo wa ushuru, ukiukaji wa haki za binadamu na kukandamiza uhuru wa kujieleza.’

Jumapili, Dkt Ruto aliahidi kuchangia ujenzi wa makanisa kadhaa huko Soin Sigowet, Bureti, Ainamoi, Kipkelion Mashariki, Kipkelion Magharibi na Belgut, kufuatia ombi la viongozi – lakini hakutaja kiasi ambacho atatoa.

Rais Ruto alisisitiza kuwa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF) ilikuwa imelipa Sh5 bilioni zilizosalia kwa hospitali nchini na nyingine Sh3.7 bilioni zitalipwa wiki hii ili kumaliza malimbikizi ya madeni.

Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA