Habari za Kitaifa

Somalia yajiunga rasmi na EAC  

March 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CHARLES WASONGA

JUMHURI ya Somalia sasa imejiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baada ya kuwasilisha rasmi stakabadhi zake za uidhinishwaji wa uanachama wake katika makao makuu ya jumuiya hiyo jijini Arusha, Tanzania.

Rais wa Somalia Sheikh Mohamud Jumatatu, Machi 4, 2024 aliongoza ujumbe wa serikali yake kuwasilisha stakabadhi hizo kwa Katibu Mkuu wa EAC Peter Mathuki.

Taifa hilo sasa litakuwa mwanachama wa nane wa jumuiya hiyo.

Mataifa mengine wanachama ni Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

“Hatua ya Somalia kujiunga na EAC sasa ina maana kuwa taifa hilo litashiriki kikamilifu katika shughuli zote za jumuiya hii kwa mujibu wa sheria ya kuundwa kwake na kanuni za uendeshaji mipango yake,” ikasema taarifa kutoka makao makuu ya EAC, Arusha.

Naye Spika wa Bunge la EALA Joseph Ntakirutimana aliwaambia wanahabari jijini Nairobi kwamba Somalia sasa itakuwa huru kuteua wawakilishi wake tisa bungeni.

“Taifa la Somalia sasa litaanza mchakato kuteua wawakilishi wake tisa katika bunge la EALA kwa mujibu wa sheria zinazoongoza shughuli hiyo. Kwa mfano, angalau thuluthi moja ya wawakilishi hao sharti wawe wa jinsia tofauti na uteuzi huo uwakilishe hata watu wasio wanasiasa,” Bw Ntakirutimana akaambia wanahabari Jumatatu katika majengo ya bunge.

Wabunge wa EALA wako Nairobi kuhudhuria vikao vya bunge hilo vitakavyodumu kwa muda wa wiki tatu, Machi 20, 2024.

Spika Ntakirutimana alieleza kuwa miswada, hoja na maombi kadhaa yameratibiwa kushughulikiwa katika vikao hivyo.

Rais wa Kenya William Ruto anatarajiwa kuhutubia bunge hilo katika ukumbi wa County ambako litaendesha shughuli zake.

Kikao cha EALA kinafanyika Kenya kwa mujibu wa Kipengele cha 55 cha Mkataba uliobuni jumuiya ya EAC, kinachosema kuwa vikao hivyo vitafanyika kwa njia ya mzunguko katika mataifa wanachama.

Mara ya mwisho kwa kikao cha EALA kufanyika Nairobi, Kenya ilikuwa mwaka wa 2018.