Habari za Kitaifa

Sonko aliahidiwa hongo ya Sh5 milioni kwa siku kuruhusu kandarasi iendelee, afisa afichua

Na RICHARD MUNGUTI July 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

AFISA mmoja wa polisi amedai kuwa Mkurugenzi wa JamboPay (Webtribe Ltd), Bw Danson Muchemi, alijaribu kumhonga aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko kwa hadi Sh5 milioni kila siku ili aendelee na kandarasi ya kukusanya mapato katika Kaunti ya Nairobi.

Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkuu Charles Ondieki katika Mahakama ya Ufisadi jana, Inspekta Mkuu Kiptoo Kisorio ambaye kwa sasa ni Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Hulugho, Kaunti ya Garissa alieleza kwa kina jinsi operesheni ya siri ilivyofanyika eneo la Mtwapa mnamo Januari 2019 kuhusu njama hiyo ya hongo.

“Mheshimiwa, nakumbuka kwamba mnamo Januari 10, 2019, saa tano asubuhi, nilitakiwa kufika ofisini kwa Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Jinai Mtwapa. Huko nilikutana na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko,” alisema Inspekta Mkuu Kisorio.

Afisa huyo aliambia mahakama kuwa Sonko alikuwa ameripoti katika kituo cha polisi cha Mtwapa kuwa alishuku Muchemi alitaka ku jaribu kumhonga ili aweze kuendelea na kandarasi ya ukusanyaji wa mapato jijini Nairobi.

Gavana huyo alitafuta msaada wa polisi kurekodi mazungumzo ya hongo kati yake na Muchemi aliyemtembelea nyumbani kwake Kanamai, Kaunti ya Kilifi.

“Gavana alisema kuwa Muchemi alitarajia kumtembelea nyumbani kwake Kanamai. Alitaka msaada wetu kumkamata ikiwa angejaribu kumpa hongo,” alieleza Inspekta huyo.

Ripoti ya kituo cha polisi (OB) yenye nambari 35/10/01/2019 iliandikishwa katika kituo cha polisi cha Mtwapa kabla ya Sonko kupewa kifaa cha kurekodi sauti aina ya Sony ICD-PX 470 (nambari ya kifaa 1161788) ili kunasa mazungumzo hayo kwa siri.

Maafisa wa polisi walimuelekeza Gavana Sonko jinsi ya kutumia kifaa hicho na wao wakajificha katika chumba kingine wakati wa kikao hicho.

“Tulimwagiza Gavana arekodi kila kitu. Mkutano huo ulidumu kwa muda, na wakati fulani mtu mwingine ambaye simfahamu aliingia na kutoka haraka. Baada ya mkutano, Gavana alitukabidhi kifaa hicho cha kurekodi,” alieleza Kisorio.

Aliendelea kusema kuwa alisikiliza rekodi hiyo baadaye katika kituo cha polisi cha Mtwapa.

“Kilichonishangaza ni jinsi Muchemi alimwambia Gavana waziwazi kuwa ikiwa angekubali kushirikiana naye, angekuwa akipokea kati ya Sh 4 milioni  hadi  5 milioni kila siku. Pia alidai kuwa aliyekuwa Gavana Evans Kidero alipata Sh7 bilioni kupitia mkataba huo wa ukusanyaji wa mapato,” alieleza afisa huyo.

Kesi inaendelea…