Spika: Sioni haja ya kuita wabunge kuangalia hoja ya Rais ya kukataa mswada
WABUNGE hawatakuwa na kikao maalum kushughulikia mapendekezo ya Rais William Ruto kuhusu Mswada tata wa Fedha wa 2024 uliokataliwa na Wakenya na kuchangia wao kuvamia majengo ya Bunge Jumanne.
Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula, aliyepokea memoranda kuhusu sababu zilizochangia Rais kukataa mswada huo Jumatano, anatarajiwa kujulisha kila mmoja wa wabunge 349 kuhusu maana ya hatua ya Rais.
Kulingana na sheria za bunge, endapo taarifa itapokewa kutoka kwa Rais, wakati ambapo wabunge wako likizoni, Spika atahakikisha kuwa taarifa hiyo inafikia kila mmoja wao.
Baadaye ataripoti ujumbe huo kwa kikao cha Bunge lote wabunge watakaporejea kutoka likizoni.
Hii ina maana kuwa memoranda kutoka kwa Rais inayowaomba wabunge kufuta sehemu zote za Mswada wa Fedha wa 2024 itashughulikiwa kuanzia Julai 22, wabunge watakaporejea kutoka likizoni.
Wabunge walianza likizo yao ya wiki tatu Alhamisi wiki hii.
“Baada ya ujumbe kupokewa kutoka kwa Rais, utachukuliwa kuwa umefikishwa rasmi bungeni na Spika anaweza kuusoma.
Wabunge walianza likizo yao baada ya kuidhinisha hoja inayoruhusu kutumwa kwa wanajeshi wa KDF kusaidia polisi kukabili vijana wanaoendelea kuandamana hata baada ya Rais Ruto kukataa kutia saini Mswada wa Fedha.
Memoranda yenye mapendekezo
Mswada huo ungekuwa sheria baada ya siku 14 endapo Rais asingeurejesha bungeni na memoranda yenye mapendekezo kwamba sehemu zake zote zifutiliwe mbali.
Ujumbe wa Rais ambao ulipokewa na Bw Wetang’ula Jumatano jioni umechukuliwa kwamba umefikishwa katika Kamati ya Bunge kuhusu Fedha ili iushughulikie.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Molo Kuria Kimani inatarajiwa kuwasilisha ripoti kuhusu ujumbe huo wa Rais Bunge litakaporejelea vikao vyake vya kawaida mnamo Julai 22, 2024.
Wabunge watahitajika kupiga kura kuhusu pendekezo la Rais kwamba sehemu zake zote zifutiliwe mbali, moja baada ya nyingine.
Endapo kuna mbunge ambaye atataka sehemu fulani ya Mswada huo isifutwe, atahitaji kupata uungwaji mkono kutoka kwa angalau thuluthi mbili ya wabunge wote, yaani wabunge 233.
Baada ya sehemu zote za Mswada huo kufutiliwa mbali, zinaweza tu kurejeshwa baada ya miezi sita.
Mswada huo tata ulikuwa umeratibiwa kuwa sheria kufikia Juni 30 na kuanza kutumiwa Julai 1, 2024 hadi Juni 30, 2025.
“Ninakataa kutia saini Mswada wa Fedha wa 2024 na ninaurejesha ili ushughulikiwe kwa kuondolewa sehemu zake zote,” Dkt Ruto akasema kwenye memoranda aliyoituma Bungeni Jumatano jioni.
Serikali ilikuwa ikitegemea mswada huo kukusanya Sh347 bilioni katika Mwaka wa Kifedha wa 2024/2025 ili kuziba mapungufu katika Bajeti ya Serikali ya kima cha Sh3.92 trilioni.
Ikiwa wabunge watafuta sehemu zote za Mswada wa Fedha wa 2024, serikali itaendelea kutumia mikakati ya kukusanya ushuru iliyoko katika Sheria ya Fedha ya 2023 iliyopitishwa Juni 24, mwaka jana.