• Nairobi
  • Last Updated June 15th, 2024 1:54 PM
Stanbic yashirikiana na Orion kuboresha mifumo ya huduma za benki

Stanbic yashirikiana na Orion kuboresha mifumo ya huduma za benki

NA HASSAN WANZALA

BENKI ya Stanbic imeanza kuboresha mfumo wake wa utoaji wa huduma unaofahamika kama Temenos 24 (T24) katika mchakato ambao utakamilika ifikapo mwishoni mwa mwaka 2024.

Ikishirikiana na kampuni ya Orion Innovation, Stanbic inalenga kuwa na mfumo wa kisasa wa huduma za benki.

Kupitia uboreshaji huu, benki hii itakuwa na mitambo na teknolojia ya kisasa inayosaidia kuongeza kasi na katika uvumbuzi endelevu ili kuwapa wateja huduma bora zaidi.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Stanbic nchini Kenya na Sudan Kusini Dkt Joshua Oigara alisema teknolojia na uvumbuzi ni nguzo muhimu kwa ukuaji wa benki hiyo katika mazingira ya kisasa ambapo operesheni zinaendeshwa kidijitali huku kukiwa na ushindani mkali.

“Usasishaji wa mitambo na huduma unapiga jeki uwezo wetu wa kiteknolojia na pia kutupa fursa ya kuhudumia wateja wetu ama wa nchini au wa kimataifa,” akasema Dkt Oigara wakati wa kutiwa saini makubaliano kati ya Stanbic na Orion Innovation katika Innovation Hub-Kilimani jijini Nairobi mnamo Jumanne.

“Hii ndio maana tunajivunia ushirikiano wetu na Orion, na bila shaka tunalenga kunufaika kutokana na ujuzi wao katika masuala ya uboreshaji wa mitambo,’’ akaongeza.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia katika benki ya Stanbic nchini Kenya Bw Alex Siboe alisema benki hiyo imejitolea kikamilifu kupiga jeki mkakati wa kuboresha namna inavyotoa huduma kwa wateja kuendana na teknolojia ya kisasa.

“Mkakati huu unawiana na lengo letu la kuwapa wateja huduma za kipekee zenye faida sufufu, na ndio maana tunajizatiti kupata teknolojia nzuri kwa nia hiyo ya kuhakikisha wateja wanaridhika,” akasema Bw Siboe.

Mbali na kukumbatia teknolojia kikamilifu, uboreshaji huo utaiwezesha benki hiyo kutoa huduma za kiubunifu kwa wateja wake, huduma zinazokidhi mahitaji yao yanayobadilika katika enzi ya kisasa ya kidijitali.

Orion Innovation inayofanya biashara kama Banktech Software Services Ltd, ambayo ni kampuni ya Amerika, iliahidi kusaidia benki hiyo kufaulu katika azma yake.

Orion ina uwezo mkubwa wa kutoa suluhu za teknolojia ya kisasa kwa kampuni kuanzia kwa mikakati, kubuni mifumo ya kufanikisha kazi, na utaalamu wa kiuhandisi.

Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Masuala ya Kifedha cha Orion barani Afrika Anoop Gala alisema lengo lao kuu ni kusaidia benki na watoaji wengine wa huduma za kifedha barani kuibuka na ubunifu wa kidijitali.

“Hii dili ni kiashirio kwamba tumejitolea kusaidia ukuaji wa sekta ya masuala ya kifedha barani Afrika,” akasema Bw Gala.

Naye Bw Suchen Janjale, ambaye anaongoza kitengo cha Masuala ya Kifedha cha Orion katika bara Ulaya alisema huduma za kiujumla zilizo ndani ya mfumo wa Temenos zilivutia Stanbic kusaka huduma zao.

“Hii pia ilichangiwa na kufaulu kwetu katika Nyanja hii ya uboreshaji wa mifumo ya benki,” akasema Bw Janjale.

Benki ya Stanbic Kenya ni mwanachama wa Standard Bank Group, benki kubwa zaidi barani Afrika kwa kiwango cha uwekezaji, inayohudumu katika nchi 20 za Afrika, pamoja na vituo vinne vya kifedha vya kimataifa na vituo viwili katika maeneo ambako hakuna tawi lolote la Stanbic.

Benki hiyo inajivunia historia ya miaka 162 katika bara la Afrika.

Mwanahisa mkubwa zaidi wa Standard Bank Group ni Benki ya Viwanda na Biashara ya China (ICBC), benki kubwa zaidi duniani, ikiwa na hisa asilimia 19.4.

Vilevile, Standard Bank Group na ICBC zinashirikiana kimkakati kurahisisha mtiririko wa biashara na ufaulishaji wa dili za kibiashara kati ya Afrika, China na masoko mateule yanayoinukia.

Nchini Kenya, Stanbic inajivunia historia ya zaidi ya miaka 100. Ni mojawapo ya benki zinazofanya vizuri nchini, ikitoa huduma zote rasmi zinazotambulika za masuala ya kifedha.

  • Tags

You can share this post!

Maswali ya KCSE kuhusu mada ya ‘Ngeli za Nomino’

Mung’aro aagiza kufungwa kwa chekechea zote Kilifi...

T L