Mkenya Stephen Munyakho aliyeepuka kunyongwa Saudia kurejea Kenya
STEVEN Bertrand Munyakho, Mkenya ambaye alikuwa akikabiliwa na hukumu ya kifo nchini Saudi Arabia, sasa ameachiliwa rasmi kutoka kizuizini.
Munyakho, kwa jina maarufu la Stevo, mwana wa kwanza wa mwandishi mkongwe Dorothy Kweyu, aliachiwa huru Jumanne saa nne asubuhi, kwa mujibu wa Katibu wa Wizara ya Masuala ya Kigeni, Korir Sing’oei. Tukio hilo liliashiria mwisho wa zaidi ya muongo mmoja gerezani.
“Steve Abdukareem Munyakho, raia wa Kenya ambaye alikuwa katika hatari ya kunyongwa katika Ufalme wa Saudi Arabia, sasa ni huru kuanzia saa nne asubuhi leo, kufuatia kutimizwa kwa masharti ya mahakama kikamilifu,” alisema Bw Korir Sing’oei kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter).
“Ubalozi wetu mjini Riyadh umethibitisha kuwa Steve alitekeleza ibada ya Umra mara tu baada ya kuachiliwa. Tutatoa taarifa zaidi kuhusu kurejea kwake nchini,” akaongeza, akiwasifu wote waliotoa mchango wao kuhakikisha mafanikio haya.
Kwa miaka mingi, hatari ya kunyongwa ilimwandama Munyakho. Kila alfajiri ndani ya Gereza la Shimeisi huko Riyadh, mustakabali wake ulionekana kuzidi kuwa mgumu hadi juhudi za wahisani na kampeni ya familia yake zikabadilisha mkondo wa mambo.
“Mwezi Machi ulipopita, nilikuwa na hofu kubwa,” aliambia Taifa Leo awali. “Michango ilianza vizuri, lakini baadaye ikazorota kabisa. Tulikuwa tukipokea hadi Sh100 pekee kwa siku, shukrani kwa Bi Florence Awimbo ambaye tangu mwanzo wa mchango huo, alituma mia moja kila siku. Sijawahi kukutana naye ana kwa ana, lakini ukarimu wake ulinilazimu kumpigia simu baada ya kupata nambari yake ya simu kupitia mchango wake.”
Kisha ikatokea habari isiyotarajiwa. Jamii ya Kiislamu Duniani (Muslim World League) ilitangaza kuwa imelipa fidia ya damu ya Sh129 milioni iliyohitajika kumkomboa Stevo jambo lililowashangaza jamaa zake, waliokuwa tayari wameanza mpango mpya wa kuchangisha pesa baada ya kushindwa kufikia lengo la Sh150 milioni.
Stevo aliondoka Kenya mwaka 1996 kwenda Saudi Arabia kutafuta ajira, ambapo alikuwa meneja katika hoteli ya kitalii karibu na Bahari ya Shamu. Lakini mnamo Aprili 2011, ugomvi wa kazini ulisababisha kifo cha raia wa Yemen, Abdul Halim Mujahid Makrad Saleh.
Ingawa alihukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kosa la kuua bila kukusudia, mahakama ya Shariah — baada ya rufaa kutoka kwa familia ya marehemu — baadaye ilimhukumu kunyongwa. Hukumu hiyo ilitarajiwa kutekelezwa Jumatano, Mei 15, 2024.
Awali, familia ya marehemu ilitaka Sh400 milioni kama fidia, lakini baadaye walikubali Sh150 milioni kama “diyya” (fidia ya damu) kulingana na sheria za Kiislamu.
Kampeni ya Bring Back Steve iliyopigwa jeki na familia yake ilijitahidi mno kuchangisha kiasi hicho.
Mnamo Oktoba 2023, kufuatia juhudi za kidiplomasia, muda wa msamaha uliongezwa kwa mwaka mmoja, na kamati ya upatanisho ilitangaza kuwa huo ungekuwa mwisho wa subira.
“Iwapo Sh150 milioni hazitapatikana,” alisema kaimu mwenyekiti Wangethi Mwangi, “familia itaruhusu mamlaka za Saudi Arabia kutekeleza hukumu ya kifo.”
Wakati huo, katibu Korir Sing’oei alithibitisha kuwa mazungumzo na Saudi Arabia yalikuwa yakiendelea ili kuzuia utekelezaji wa hukumu hiyo.
Wakati wote wa kifungo chake, Stevo alionyesha majuto makubwa. Katika simu moja kwa mama yake, alisema: “Naomba, nawasihi, waambie: sikukusudia kuua mtu mwingine.”