• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 AM
Taarifa ya sera yalenga kuwatoza Wakenya ushuru zaidi, Azimio yaonya

Taarifa ya sera yalenga kuwatoza Wakenya ushuru zaidi, Azimio yaonya

NA CHARLES WASONGA

MUUNGANO wa Azimio La Umoja-One Kenya umeonya serikali inapanga kuwabebesha Wakenya na mzigo zaidi wa ushuru katika mwaka ujao wa kifedha.

Vinara wa muungano huo wanadai Taarifa ya Sera ya Bajeti (BPS) inayojadiliwa na wabunge wakati huu, imesheheni mapendekezo kadhaa ya nyongeza ya ushuru.

“Taarifa ya Sera ya Bajeti inayojadiliwa katika bunge wakati huu inayo habari mbaya kwa Wakenya, haswa wale wenye mapato duni. Wakenya wanafaa kukaza mikanda kwa sababu Kenya Kwanza inapanga kuwaongezea ushuru zaidi,” akasema kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

“Tumeapa kupinga nyongeza zozote za ushuru zitakazoletwa na utawala huu,” akaongeza Makamu huyo wa Rais wa zamani.

Bw Musyoka alisema hayo baada ya kuongoza mkutano wa Baraza Kuu la Azimio katika Afisi za Wakfu wa Jaramogo Oginga Odinga, mtaa wa Upper Hill, Nairobi.

Aliandamana na vinara wengine kama vile kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa, Kiongozi wa Chama cha Roots Profesa George Luchiri Wajackoyah, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni na magavana wa zamani Mwangi Wa Iria (Murang’a) na Ndiritu Muriithi (Laikipia) miongoni mwa wengine.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi.

Kulingana na taarifa hiyo ya BPS, serikali inapendekeza kuwatoza wakulima ushuru kwa malipo ya mazao watakayouza kwa vyama vya ushirika.

Hii ina maana kuwa endapo pendekezo hilo litapitishwa, wakulima watatozwa asilimia tano ya mauzo ya mazao yao kama ushuru unaojulikana kwa Kiingereza kama “withholding tax”.

Pesa hizo zitakuwa zikiwasilishwa moja kwa moja kwa Mamlaka ya Ukusanyaji wa Ushuru Nchini (KRA).

  • Tags

You can share this post!

Baba na mwanawe wa miaka 3 wauawa kwa risasi na majangili

Nadia Mukami adai MCSK inamkausha pesa za mrabaha kwa...

T L