Habari za Kitaifa

Tafuteni barakoa mvalie sababu kuna wimbi la mafua, Wakenya waambiwa

April 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ELIZABETH OJINA NA LABAAN SHABAAN

WATAALAMU wa afya eneo la ziwa – Lake Basin – wameonya kuna uwezekano wa kuongezeka kwa homa ya Influenza na Covid-19 kote nchini huku mgomo wa madaktari ukiendelea.

Vile vile, wameonya kuwa mvua kubwa inayoendelea kunyesha inaweza kuchochea msambao wa magonjwa ya kupumua.

Tayari baadhi ya taasisi za afya kupitia nyaraka rasmi, zimetoa ilani ya maambukizi haya.

Mshirikishi wa Programu ya Kamati ya Ushauri wa Covid-19 ya Ukanda wa Kiuchumi wa Lake Basin (LREB), Prof Shem Otoi Odhiambo amesema hali ya mazingira inachochea msambao wa maambukizi.

“Sababu ya hali ya baridi, mikakati yote iliyochukuliwa wakati wa mlipuko wa Covid-19 inafaa kurejelewa.

Ilivyo sasa, hali ya anga inatoa mazingira ya maambukizi ya homa ya Influenza na Covid-19,” alisema Prof Otoi.

Utafiti unaonyesha kuwa mazingira baridi husababisha maradhi ya mkondo wa hewa miongoni mwa binadamu.

Hii ni licha ya virusi kusambaa wakati wote wa mwaka, hasaa maeneo ya tropiki.

“Sisi kama LREB tunaomba Wizara ya Afya na serikali kusuluhisha mgogoro na madaktari. Hii si mara ya kwanza kwa hali hii ya vuta nikuvute. Serikali inafaa kuwa na uaminifu katika mashauriano na madaktari,” alisema Prof Otoi.

Alieleza kuwa serikali ina jukumu la kutimiza haki ya wananchi.

Kadhalika alisema iwapo serikali italegea, Wakenya watataabika.

Hofu ya maambukizi inaibuka katika kipindi ambacho aina mpya ya Covid-19 inayoitwa JN1 imegunduliwa.

Wakati msimbo huo uligunduliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mnamo Disemba 2023, shirika hilo lilinakili kuwa haukuwa umeenea.

Virusi vya HN1 vilichipuka baada ya kubadilika kwa sababu ya viwango vikubwa vya virusi na viliathiri watu waliombukizwa na misimbo ya Covid-19.

Dalili za aliyembukizwa zinahusisha kukohoa, uchovu, mkazo wa kupumua na kifua.

Hata hivyo, inatofautiana kidogo na aina nyingine katika maradhi ya kuendesha na maumivu ya tumbo.

WHO imeshauri mataifa kuchukua tahadhari msimu wa baridi ili kuzuia maambukizi ya homa.

Hata hivyo, Wizara ya Afya imepinga ripoti ya kupanda kwa visa vya Covid-19 vinavyosababishwa na aina mpya ya virusi.

 “Tunashikilia kwa nguvu kuwa kuna maambukizi ya Covid-19 yanayoendelea katika mwezi mmoja uliopita, bila historia yoyote ya usafiri. Hii inamaanisha maambukizi ni ya humu nchini, hayajaingia kutoka nchi nyingine,” alihakikisha Prof Otoi.

Kiongozi wa Afya wa LREB Ochieng Gumbo hata hivyo ameomba wananchi kuvaa barakoa, kusafisha mikono na kufuata kanuni ya umbali ili kuepuka maambukizi.