Tambua kwa nini Rais hana mamlaka kikatiba kuondoa mswada ambao umepitishwa na wabunge
JAPO Rais William Ruto ametangaza Jumatano kuwa ameuondoa Mswada wa Fedha wa 2024 baada ya Wakenya kuukataa, hana mamlaka ya kufanya hivyo kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Bunge.
Kwa mujibu wa Kipengele 115 cha Katiba, kile Rais anaweza kufanya ni kuurejesha mswada huo bungeni akiuandamanisha na mapendekezo kuhusu sehemu ambazo hakubaliani nazo.
“Baada ya mswada wowote kuwasilishwa kwa Rais, (a) ..atautia saini kuwa sheria au (b) .. ataurejeshe bungeni na mapendekezo kuhusu sehemu ambazo angetaka wabunge wazifanyie marekebisho kabla ya kurejeshwa kwake tena,” inasema kipengele hicho.
Kwa kuwa Wakenya, haswa vijana wa kizazi cha Gen-Z wameukataa Mswada huo, kile Rais Ruto anaweza kufanya sasa ni kuurejesha bungeni akiiandamanisha na memoranda inayopendekeza kuwa sehemu zote za mswada huo zifutiliwe mbali.
Hii ina maana kuwa wabunge ambao wameenda likizoni, wataitwa kwa kikao maalum kwa ajili kupitisha pendekezo hilo la Rais Ruto.
Lakini, kulingana na kipengele hicho cha 115 cha Katiba, endapo Rais atanyamaza bila kufanya lolote, mswada huo utakuwa sheria baada ya siku 14.