Tanzania yakataza raia wa Kenya kushiriki biashara ndogo ndogo nchini humo
UAMUZI wa Tanzania wa kulinda biashara ndogo ndogo dhidi ya raia wa kigeni umeibua mzozo mkubwa unaoweza kuwa kikwazo kipya kisicho cha ushuru katika biashara huru kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Kawaida, raia wa nchi wanachama wa EAC kama Kenya, Uganda, na Tanzania wana uhuru wa kuvuka mipaka yao kuanzisha biashara ndogo ndogo kama saluni, huduma za kutuma na kutoa pesa kwa simu, utengezaji wa simu na kuongoza watalii, mradi wawe na leseni zinazohitajika.
Lakini Tanzania, chini ya shinikizo la kujenga fursa za kiuchumi kwa raia wake karibu 60 milioni, imezuia raia wa kigeni kuendesha biashara hizo.
Kulingana na Wizara ya Bishara na Viwanda ya Tanzania, sera hii ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kukuza ukuaji unaoongozwa na raia, kupanua fursa za kiuchumi kwa Watanzania, na kubadilisha muundo wa umiliki wa biashara za ndani.
Hata hivyo, hatua hii inaweza kuathiri biashara za EAC na huenda nchi zinazohusika zikazima Watanzania pia.
Angalau Wakenya 40,000 wanaishi na kufanya kazi Tanzania, ingawa idadi halisi ya wanaohusika na biashara zisizo rasmi kama saluni haijulikani wazi.
Nchi nyingine za EAC zinazojihusisha na sekta isiyo rasmi ni Rwanda, Burundi, Somalia, Sudan Kusini, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Siku moja baada ya sera hiyo kutangazwa, wadau nchini Kenya walilaumu Tanzania kwa kuweka vikwazo kwa makubaliano kati ya nchi hizo mbili ya kurahisisha biashara.
Mwenyekiti wa Chama cha Utalii Pwani Kenya (KCTA), Bw Victor Shitakha, alisema hatua hiyo inaweza kuwadhuru Wakenya wanaotoa huduma za utalii Tanzania.
“Tangu 2020, kumekuwa na shida ya magari ya watalii kutoka Kenya kuingia Tanzania na hivi karibuni nchi jirani ilijaribu kuzuia ndege za Kenya Airways nchini humo. Tangazo hili ni kinyume na itifaki ya EAC inayoruhusu uhuru wa kusafiri na kusafirisha mizigo katika ukanda,” alisema Bw Shitakha.
“Nchi hizi mbili zinapaswa kutatua mgogoro huu kwani wanyama hawana mipaka.”
Kenya na Tanzania kwa kawaida zimekuwa na migogoro ya biashara kwa muda mrefu, lakini tangu Desemba 2021, zilitia saini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kushughulikia matatizo hayo.
MoU hiyo ilitaja vikwazo vya biashara na pande mbili zikakubaliana kuboresha biashara za mipakani na kuruhusu ushirikiano wa rasilmali asilia kwa kuondoa vizuizi vya uhamiaji.
Uamuzi huu ulijiri baada ya nchi hizo kuzuia waelekezi wa watalii wa pande zao kuendesha huduma katika nchi jirani na kusitisha safari za ndege.
Dkt Sam Ikwaye, Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Wamiliki na Wahudumu wa Hoteli (KAHC), alisema nchi hizo mbili zinapaswa kuendeleza ushirikiano.
“Tunasubiri kuona kama Kenya itapewa nafasi maalum katika tangazo hili kwa kuzingatia makubaliano mengi tuliyonayo na Tanzania,” alisema Dkt Ikwaye.
Kenya haikutoa jibu mara moja kwa amri mpya iliyotolewa na Wizara ya Viwanda na Biashara Tanzania inayoruhusu baadhi ya biashara kuwa maalum kwa Watanzania pekee, ikiwa ni pamoja na migodi midogo na biashara za mali isiyohamishika.
Tanzania pia imesitisha wakulima kuuza mazao yao moja kwa moja kwa raia wa kigeni shambani.
Agizo la Leseni za Biashara (Kuzuia Biashara kwa Watu Wasio-raia), 2025, lililotolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt Selemani Saidi Jafo, linakataza raia wa kigeni kushiriki katika aina 15 za biashara, kuanzia biashara ya jumla, utoaji wa huduma, vyombo vya habari, utalii, na viwanda vidogo.
“Baada ya agizo hili kuanza kutumika, mamlaka za utoaji wa leseni hazitakiwi kutoa leseni kwa mtu asiye raia kufanya shughuli zozote zilizokatazwa kupitia agizo hili,” alisema Jafo.
Hata hivyo, wale waliokuwa na leseni halali wataruhusiwa kuendelea na biashara hadi leseni zao zitakapokamilika.