Tanzia: Kamishna wa Lamu, Louis Rono aaga dunia
NA KALUME KAZUNGU
KAMISHNA wa Kaunti ya Lamu Louis Rono ameaga dunia wakati alikuwa akipokea matibabu mapema Alhamisi katika hospitali moja mjini Bomet.
Akithibitisha, Kaimu Kamishna wa Lamu Charles Kitheka alisema afisa huyo alikuwa akifanyiwa operesheni lakini akafariki.
“Ni masikitiko kwamba tumempoteza Kamishna wetu Louis Rono. Alifariki akifanyiwa upasuaji huko Bomet. Mola ailaze roho yake mahali pema peponi,” akasema Bw Kitheka.
Mmoja wa mawaziri wa zamani wa Kaunti ya Lamu, Paul Thairu, alimtaja Rono kuwa wakati wa uhai wake, alikuwa mtu mnyenyekevu na mpenda wote.
“Nimepokea habari za kifo cha kamishna Rono kwa majonzi tele. Ni mmojawapo wa makamishna wangwana waliowahi kuhudumia eneo hili la Lamu. Alikuwa mpole, mwenye utu, mpenda amani na mwenye kujituma kazini. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi,” akasema Bw Thairu aliyewahi kuhudumu kama Waziri wa Elimu na Jinsia kaunti ya Lamu.
Mwenyeji wa Lamu, Bw Francis Mugo alimtunuka sifa kamishna Rono, akimtaja kuwa kiongozi jasiri, mwenye hekima na ambaye alichukia ukabila hasi.
Rono aliwahi kuhudumu kama Naibu Kamishna wa Lamu Magharibi kabla ya kuhamishwa hadi sehemu nyingine.
Mnamo 2023, alipandishwa cheo na kurudishwa tena Lamu kama Kamishna kamili wa kaunti hiyo, jukumu ambalo alilitekeleza hadi kifo chake.
Atakumbukwa kwa kupigana vita vikali dhidi ya ugaidi akilenga Al-Shabaab waliokuwa wakitesa Lamu.
Utulivu na amani inarejea eneo hilo hadi sasa, ishara tosha alifanya kazi yake kwa njia nzuri.