Tekinolojia ilivyookoa Gavana Mutai kwa mara ya pili katika seneti
Gavana wa Kericho, Erick Mutai, alinusurika kung’olewa mamlakani kwa mara ya pili baada ya Seneti kuingilia kati dakika za mwisho – na kwa mshangao wa wengi, ni teknolojia iliyomuokoa.
Katika mchakato uliogubikwa na utata, mjadala mkubwa ulijikita katika mfumo wa kura za dijitali uliotumiwa na Bunge la Kaunti ya Kericho. Mfumo huo ulizua maswali kuhusu uhalali wa kura 33 zilizopigwa dhidi ya Mutai. Baadhi ya Madiwani walidai hawakupiga kura, ingawa rekodi ya mfumo ilionyesha walishiriki.
Wataalamu wa teknolojia waliotoa ushahidi mbele ya Seneti waligawanyika. Ripoti ya Mamlaka ya ICT ilisema kuwa mfumo huo haukuweza kuruhusu mtu kupigia kura kwa niaba ya mwingine.
Hata hivyo, ripoti hiyo ilikumbwa na mashaka makubwa kwa kuwa iliwasilishwa bila saini ya upande wa Gavana, ilionyesha kuwa anwani moja ya intaneti ilitumiwa kupiga kura mara tisa, ilikosa ushahidi wa mafunzo kwa Madiwani kabla ya matumizim ilibainika kuwa mfumo uliwekwa usiku kabla ya kura kupigwa na mtaalamu aliyekuwa amefutwa kazi na serikali ya Mutai.
Wataalamu wengine walibaini kuwa mfumo huo ulikuwa na dosari za kiusalama, na uwezekano wa mtu kupiga kura kwa niaba ya mwingine endapo angepata nambari ya kitambulisho cha mhusika.
Kwa msingi huu, baadhi ya Maseneta walisisitiza kuwa haikuwa haki kumwondoa gavana kwa kutumia mfumo usio na uhakika, usiokaguliwa kikamilifu, na uliowekwa kwa haraka isiyokuwa ya kawaida.
Seneta Jackson Mandago alieleza kuwa mfumo huo ulikuwa “gari la dharura” lililoundwa kwa lengo moja: kumtimua Gavana. Seneta Godfrey Osotsi naye alisema mfumo huo haukidhi vigezo vya Katiba chini ya Kifungu cha 86 kuhusu kura kuwa ‘rahisi, sahihi, salama, na ya kuaminika.’
Seneti iliamua kumpa Mutai nafasi ya pili, si kwa sababu hakuwa na makosa, bali kwa sababu njia ya kumuondoa ofisini ilionekana kuwa na shaka kubwa.