• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
TikTok yatoa mwongozo mpya kuzima habari potoshi

TikTok yatoa mwongozo mpya kuzima habari potoshi

NA KABUI MWANGI

TIKTOK inayovuma kwa kuwapa watengenezaji maudhui jukwaa la kupakia video zao mtandaoni, imezindua mwongozo mpya katika jitihada za kuzuia kuenea kwa matamshi ya chuki na habari za kupotosha umma.

Sera mpya inayoanza kutumika kuanzia mwezi huu wa Mei, inaweka wazi kuwa mpakiaji maudhui ambaye atagundulika kuwa na mazoea ya kuchapisha maudhui yanayokiuka vigezo vilivyowekwa, atasukumwa nyuma ya pazia.

Hii inamaanisha kwamba ujumbe wake utatolewa kwa muda kwenye sehemu ya ‘Kwa Ajili Yako’, kumaanisha kuwa itakuwa vigumu wafuatiliaji kupata maudhui ya mtayarishaji husika katika sehemu ya utafutaji.

Hata hivyo, TikTok itawafahamisha wamiliki wa akaunti zitakazowekewa vikwazo vya aina hii, watajulishwa na kupewa nafasi ya kukata rufaa.

Katika mwongozo huu mpya, mtayarishi anayekiuka sera kwa mara ya kwanza atapokea onyo na ataarifiwa kuhusu sheria ambayo amekiuka na jinsi anavyoweza kukata rufaa iwapo anaamini kuwa amehukumiwa kimakosa.

“Onyo la kwanza kabisa kuhusu ukiukaji mwongozo halitahesabika, lakini ukiukaji wowote wa siku zitakazofuata, utazingatiwa. Makosa yasiyoweza kuvumiliwa (kwa mfano, uchochezi wa vurugu) yatatolewa hukumu moja kwa moja bila vikumbusho ambapo akaunti husika zitapigwa marufuku mara moja,” TikTok ikasema.

Aidha kampuni ya ByteDance inayomiliki TikTok pia iliongeza kipengele kipya kinachoitwa ‘Kukagua Akaunti’ ambacho kitawaruhusu watayarishaji wa maudhui kuangalia hali ya akaunti zao na kukagua machapisho yao 30 ya mwisho ili kubaini kuwa wanatii vigezo vya kukubalika na program hiyo.

“Kukagua Akaunti pia kutajumuisha maelezo kuhusu iwapo ufikiaji wa vipengele fulani, kama vile maoni au ujumbe wa moja kwa moja, umezuiwa kwa sababu ya ukiukaji. Watayarishaji maudhui pia wataweza kuona ikiwa kazi zao zimeondolewa kwa kukiuka sheria zetu au zimezimwa kuwa kwa sehemu ya Kwa Ajili Yako,” ikasema.

TikTok katika siku za hivi majuzi imekuwa ikisutwa na kupokea upinzani mkubwa, haswa nchini Amerika ambapo Rais Joe Biden ametia saini kuwa sheria mswada ambao unalenga kuipiga marufuku nchini humo au ByteDance iiuze ndani ya mwaka mmoja.

Kutiwa saini kwa mswada huo wiki iliyopita kulitokana na madai kwamba jukwaa hilo linalomilikiwa na kampuni hiyo ya China, linafanyia serikali ya China kazi ya kukusanya na kutumia kisiri data za watumiaji.

Hatua hiyo ya Amerika ilijiri wakati ambapo Kenya imejiunga na orodha inayozidi kukua, ya mataifa yanayotaka kudhibiti TikTok katika jaribio la kupambana na habari za uongo, habari potoshi na ulaghai pamoja na usambazaji wa maudhui ya ngono.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Linturi pabaya hoja ya kumtimua ikipita Bungeni

Waasi wa M23 wadhibiti eneo la madini ya kutengenezea...

T L