Habari za Kitaifa

Tofauti ya Linda Mama na Linda Jamii yajitokeza: ‘Sikulipa chochote’ na ‘Nilizuiliwa sababu ya bili’

Na MERCY CHELANGAT October 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MIAKA 10 iliyopita, Gladys Midecha alipogundua kuwa ana ujauzito, alienda kutafuta usaidizi katika kliniki ya kaunti ya jiji iliyokuwa karibu naye.

Alipoulizwa kama alikuwa amejiandikisha kwa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF) iliyokuwa ikifanya kazi wakati huo, alilipa Sh20, akapokea kijitabu cha kliniki, na kuandikishwa katika mpango wa Linda Mama.

Kupitia mpango huo, huduma zote za kliniki alizopokea zilikuwa bure. Akiwa hana ajira wakati huo, chaguo lake bora lilikuwa kliniki hiyo.

Alipokea chanjo zote tatu za pepopunda bila malipo na alifanyiwa vipimo vya virusi vya HIV bila kulipa.

“Kwa akina mama waliopatikana na virusi vya HIV, kliniki iliwapa ushauri nasaha na dawa bila malipo. Madaktari na wauguzi walijitolea sana. Kila ziara ya kliniki walituambia cha kutarajia, walipima uzito, urefu, na hata kutupa ushauri kuhusu lishe,” akaeleza.

Huduma pekee ambayo haikupatikana katika kliniki hiyo ilikuwa picha (ultrasound). Hivyo, alipofikisha miezi saba, alilipa binafsi kupata picha ya kuona hali ya mtoto.

Mkewe Kinara wa Mawaziri Tessie Mudavadi alipotembelea kina mama waliojifungua awali mnamo 2023 chini ya mpango wa afya wa Linda Mama. Mpango huo uliondolewa baadaye na kuanzishwa Linda Jamii chini ya SHA. Picha|Lucy Wanjiru

Mnamo Oktoba, alitembelea Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta kujifungua. Alikaguliwa, akaombwa kitabu cha Linda Mama na akalazwa.

“Nilijifungua salama na nilitoka hospitalini asubuhi iliyofuatia. Sikulipa hata shilingi moja. Kitabu cha kliniki ndicho kilikuwa muhimu pekee,” asema.

Lakini miaka 10 baadaye, Melvin Nyaoga alipitia hali tofauti kabisa.

Mwezi mmoja uliopita, alianza kupata dalili za uchungu wa kujifungua kabla ya tarehe aliyotarajia.

Kituo cha afya alichotembelea kilimwelekeza kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mafunzo ya Moi (MTRH) baada ya maji ya uzazi kuanza kutoka.

Alipofika MTRH saa tano asubuhi, aliambiwa alipe Sh520 za kutengewa kitanda. Hakuwa na pesa, hali iliyosababisha kuchelewa kulazwa.

Alingoja hadi saa 11 jioni, akitokwa na maji ya uzazi kwa saa sita.

Asubuhi iliyofuata, alifanyiwa upasuaji wa dharura na kujifungua salama. Hata hivyo, matatizo ya kifedha yaliongezeka, mtoto wake akilazwa katika kitengo cha watoto wachanga kwa uangalizi maalum.

“Wakati wa kulipia hospitali, niliambiwa nilipe mwaka mzima wa bima ya SHA ndani ya saa 24 baada ya kujifungua, ili nisaidiwe kulipa bili ya hospitali. Nilikuwa nimeambiwa awali kuwa naweza kulipia miezi minne tu. Sasa niliambiwa lazima nilipe mwaka mzima, na nilikuwa nimechelewa. Bili yangu kwa siku mbili tu ilikuwa tayari imefikia Sh72,000,” alisema.

“Mtoto wangu alikaa katika chumba cha uangalizi wa watoto wachanga kwa siku 11, na kuongeza bili ya Sh18,000. Kwa kuwa hosteli ya hospitali ilikuwa imejaa, tuliendelea kukaa wodini. Niliruhusiwa kuondoka wiki mbili zilizopita baada ya kuandamana hospitalini kwa sababu ya kuzuiliwa kwa kushindwa kulipa deni,” anaeleza.

Waliyopitia Gladys na Melvin yanaonyesha tofauti kubwa ya huduma ya uzazi kwa akina mama wasio na uwezo wa kifedha nchini Kenya.

Mpango wa Linda Mama ulianzishwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta mnamo Juni 2013 kama huduma ya bure ya uzazi kwa akina mama katika hospitali za umma.

Serikali baadaye ilikabidhi jukumu hilo kwa NHIF ili kuongeza ufanisi wa malipo na upanuzi wa mpango huo mwaka 2016.

Lengo kuu lilikuwa kuhakikisha kuwa wanawake wote wajawazito na watoto wao wanapata huduma bora bila vizingiti vya kifedha, na pia kusaidia katika kufanikisha Huduma ya Afya kwa Wote (UHC), kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga, na kuongeza idadi ya wanaojifungua kwa msaada wa wahudumu wa afya waliobobea.

Kwa sasa, serikali ya Rais William Ruto imeanzisha mpango mpya wa Linda Jamii, unaolenga kuendeleza mafanikio ya Linda Mama.

Mpango huu, uliozinduliwa Juni 2025, unasimamiwa na Mamlaka ya Bima ya Afya ya Jamii (SHA). Kwa mujibu wa Rais, Linda Jamii ni mpango mpana unaolenga familia nzima, si mama na mtoto tu.

Wanawake sasa wanaweza kuwasajili waume na watoto wao ili familia nzima inufaike.

Huduma zilizotolewa chini ya mpango huu zilijumuisha: huduma za kliniki kabla ya kujifungua, kujifungua kwa njia ya kawaida au kwa upasuaji, huduma baada ya kujifungua, huduma za dharura, na uangalizi wa watoto wachanga katika hali ya kawaida na ya dharura, kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu mwanzo wa usajili.

Kufikia mwaka wa 2023, zaidi ya akina mama milioni 5.2 walikuwa wamejiandikisha chini ya mpango huu, huku wastani wa milioni 1.2 wakinufaika kila mwaka kati ya 2019 na 2023. Jumla ya hospitali 5,635 za umma, 437 za binafsi na 164 za kidini zilikuwa zimesajiliwa kutoa huduma hizo.

Kwa sasa, serikali ya Rais William Ruto imeanzisha mpango mpya wa Linda Jamii, unaolenga kuendeleza mafanikio ya Linda Mama.

Mpango huu, uliozinduliwa Juni 2025, unasimamiwa na Mamlaka ya Bima ya Afya ya Jamii (SHA).

Kwa mujibu wa Rais, Linda Jamii ni mpango mpana unaolenga familia nzima, sio mama na mtoto tu. Wanawake sasa wanaweza kuwasajili waume zao na watoto ili familia nzima inufaike.

Mpango huu unajumuisha huduma za kabla na baada ya kujifungua, huduma za watoto wachanga, matibabu ya nje na ya kulazwa, na huduma za dharura.

Dkt Abdi Mohamed, mwenyekiti wa SHA, anasema changamoto kuu ya Linda Mama ilikuwa kuwa mpango wa tukio moja tu, badala ya bima kamili ya afya.

“Mpango huo haukutoa suluhisho la kina kwa akina mama waliokwama hospitalini kwa sababu ya bili,” asema.

Anasema Linda Mama ililipa Sh2,500 kwa kujifungua kawaida katika hospitali za umma, na Sh5,000 kwa upasuaji. Katika hospitali binafsi na za kidini, malipo yalikuwa Sh5,000 na Sh17,000 mtawalia—chini zaidi ya malipo ya Super Cover ya NHIF ambayo ni Sh10,000 na Sh30,000.

“Malipo haya ya chini yalisababisha baadhi ya watu kutumia mpango vibaya kwa kudai malipo mara mbili au kujifungua mara kadhaa kwa mwaka,” anaongeza.

Dkt Abdi anasisitiza kuwa mfumo mpya wa Linda Jamii ni bora zaidi kwa kuwa ni mpango wa familia mzima kwa msingi wa ada ya kila mwaka.

Anasema kuwa tatizo la akina mama kuzuiliwa hospitalini linatokana na kutosajiliwa mapema.