Habari za Kitaifa

TSC yathibitisha kuendelea kulipa marupurupu ya mazingira magumu baada ya shutuma

Na SAMWEL OWINO July 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TUME ya Huduma kwa Walimu (TSC) imesema haijapitia upya maeneo yanayotambuliwa kama ya mazingira magumu kwa walimu, ikieleza kuwa inasubiri mwelekeo kutoka kwa Tume ya Huduma za Umma.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Eveleen Mitei, aliambia Kamati ya ya Bunge la Kitaifa kuhusu Utekelezaji kwamba tume hiyo bado inalipa walimu marupurupu ya mazingira magumu kulingana na Tangazo la Kisheria Nambari 534 la mwaka 1997.

“Tunalipa marupurupu haya kwa kutumia Tangazo la Kisheria Na. 534 la 1997. Tumejulishwa kuwa Tume ya Huduma za Umma iko katika mchakato wa kupitia upya maeneo haya, lakini kwa sasa bado tunazingatia tangazo hilo,” Bi Mitei aliwaambia wabunge.

Alikuwa akijibu swali kutoka kwa mwenyekiti wa kamati hiyo, Raphael Wanjala, aliyepinga vigezo vinavyotumika katika kulipa marupurupu hayo, akisema yanaegemea upande mmoja na yamekuwa ya kibaguzi.

“Ni vigezo vipi mnatumia kutoa marupurupu ya mazingira magumu? Unaweza kuona eneo moja katika eneo bunge fulani limetambuliwa kama la mazingira magumu ilhali lingine halijatambuliwa. Walimu wanakimbilia maeneo yenye marupurupu haya, na kuacha shule nyingine bila walimu,” alisema Bw Wanjala.

“Unaona walimu wengi wamejazana shule moja, wakiketi bila kazi huku wakitumia TikTok siku nzima kwa sababu walihonga maafisa wenu walioko mashinani ili wapewe marupurupu ya mazingira magumu,” aliongeza.

Wabunge wengine pia walieleza kuwa baadhi ya shule katika maeneo yao hazina walimu kwa sababu walimu wamehamia maeneo yanayotoa marupurupu hayo.

Mbunge wa Kajiado Mashariki, Kakuta Ole Maimai, alisema shule zilizo maeneo ya miji katika eneo lake zimejaa walimu, ilhali zile za mashambani hazina hata mmoja.

Mnamo Mei mwaka huu, Mkuu wa Mawaziri aliambia Bunge kwamba serikali ilikuwa mbioni kupitia upya maeneo yanayotambuliwa kama ya mazingira magumu.

Bw Musalia Mudavadi alisema hatua hiyo ingetatua changamoto ya gharama kwa serikali na kuokoa Sh6 bilioni kila mwaka.

“Ningependa kulijulisha Bunge kuwa utekelezaji wa ripoti ya Kamati ya Kiufundi ya Mashirika ya Serikali utapunguza gharama ya malipo ya marupurupu ya mazingira magumu kutoka Sh25 bilioni hadi Sh19 bilioni kwa mwaka, na hivyo kufanya serikali kuokoa Sh6 bilioni,” alisema Bw Mudavadi.

Alikuwa akirejelea ripoti ya kamati ambayo ilifanya mashauriano ya kina na wadau kuhusu sera na mwongozo wa kutambua maeneo hayo pamoja na mfumo wa malipo ya marupurupu husika katika sekta ya umma.

Hata hivyo, mnamo Julai, Waziri wa Utumishi wa Umma, Geoffrey Ruku, alitangaza kwamba serikali imeamua kusitisha utekelezaji wa ripoti hiyo kufuatia malalamishi kutoka kwa walimu, watumishi wa umma na viongozi wa kisiasa kote nchini.

Bw Ruku alisema wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu imeamua kusitisha utekelezaji wa ripoti hiyo ili kufanya tathmini mpya na kufafanua upya maeneo yanayostahili marupurupu hayo.

TAFSIRI: BENSON MATHEKA