Tuju: Siko vizuri kumenyana na Orengo kwa ugavana 2027
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee, Bw Raphael Tuju, amepuuzilia mbali madai kuwa alijizulu chamani kuwania ugavana wa Siaya katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Akiongea katika kipindi cha Fixing The Nation kwenye runinga ya NTV jana, waziri huyo wa zamani alifafanua kuwa alijiondoa Jubilee kupata nafasi ya kuendesha biashara zake na “ili niweze kujieleza bila kudhibitiwa kisiasa.”
“Siko katika nafasi nzuri ya kuwania ugavana wa Siaya kwa sababu wakati huu nimekita Nairobi nikiendesha biashara zangu. Nikifanya uamuzi kama huo ninaweza kuvuruga maisha ya zaidi ya watu 100 niliowaajiri katika biashara hizo,” Bw Tuju akasema.
Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Rarieda alisema alijiuzulu kama mwanachama wa Jubilee kwa hiari bila kusukumwa wala kushawishiwa na mtu au jambo lolote.
“Niligura chama cha Jubilee kutoka na sababu za kibinafsi na bila hisia mbaya. Nilichukua hatua hiyo ili niweze kupata nafasi ya kutoa maoni yangu ya kibinafsi kuhusu masuala mbalimbali bila kuulizwa ikiwa nifanya hivyo kwa niaba ya mtu mwingine au chama chama cha kisiasa. Sasa ninaweza kuongea kwa niaba yangu. Kimsingi, nimeingia nafasi huru nilivyo hapa kwenye studio za NTV,” Bw Tuju akaeleza.
Aidha, alisema kuwa hana hamu ya kuhudumu katika Serikali Jumuishi wakati huu japo anaiunga mkono.
“Naunga mkono serikali jumuishi kwa sababu inalenga kuleta utulivu nchini ili pawepo na mazingira faafu kwa shughuli za kiuchumi kunawiri. Lakini sio kama nitaweza kuhudumu katika wadhifa wowote serikalini wakati kama huu,” Bw Tuju akaeleza.
Baada ya Waziri huyo wa zamani wa Mashauri ya Kigeni kutangaza kujiondoa Jubilee Agosti 19, 2025, wengi walianza kueneza uvumi kwamba analenga kuwania wadhifa wa Ugavana wa Siaya.
Gavana James Orengo anayehudumu muhula wake wa kwanza, anatarajiwa kutetea kiti hicho 2027.
Wengine walidai kuwa Rais William Ruto na mshirika wake Raila Odinga, wamemwahidi Tuju cheo fulani kubwa katika serikali jumuishi.
Kwenye barua aliyotuma kwa kiongozi wa Jubilee Rais mstaafu Uhuru Kenyatta Bw Tuju alisema hivi: “Japo ninaweza kufanyakazi nawe siku zijazo, wakati huu sioni thamani yoyote ambayo ninaweza kuongeza katika chama cha Jubilee. Kwa hivyo, najiuzulu kama mwanachama. Nakutakia ufanisi pamoja na chama cha Jubilee.”
Bw Tuju aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Masuala ya Kigeni katika serikali ya Rais wa Tatu wa Kenya Hayati Mwai Kibaki.
Aidha, alihudumu kama Waziri asiyesimamia Wizara mahsusi wakati wa utawala wa Bw Kenyatta.