Habari za Kitaifa

Tuliona tu mitandaoni: Uchungu familia ikilaumu serikali kuhusu mauti ya mwana wao Haiti

Na KEVIN CHERUIYOT September 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

FAMILIA ya afisa wa polisi Benedict Kabiru Kuria ambaye aliuawa Haiti, imelalamikia jinsi serikali ilishughulikia habari za mauti ya mwanao.

Bw Kuria alikuwa miongoni mwa maafisa wa usalama ambao walitumwa Haiti kupambana na magenge yanayohangaisha serikali ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa familia yake, habari kuhusu mauti ya mwanao zilienea mitandaoni lakini juhudi zao za kuzithibitisha kutoka kwa Tume ya Kitaifa ya Huduma kwa Polisi (NPS) hazikufaulu.

Walilalamika kuwa, walisikia habari hizo tu wakati Rais Ruto alitaja mauti hayo kwenye hotuba yake katika mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa (UN).

Akiongea na Taifa Leo Alhamisi, nduguye marehemu Philip Kuria Kamau, alisema kuwa, baada ya hotuba ya rais, maafisa wa serikali walitembelea nyumbani kwao Jumatano usiku.

“Walikuja nyumbani na kutueleza habari kuhusu mauti yake. Tulikuwa tumeona tu mitandaoni kuwa alikuwa ameaga dunia,” akasema Bw Kamau.

Alifichua kuwa familia hiyo ilikuwa imepanga kuandamana hadi Nairobi kueleza kero lao lakini maafisa wa serikali walioandamana na polisi wakawaomba wapewe muda zaidi kushughulikia maelezo yanayoandamana na mauti ya Bw Kabiru.

“Tulikuwa tumeenda kituo cha polisi cha Kikuyu lakini wakatuambia tusubiri hadi Jumanne. Hatujaridhika na maelezo ya serikali kwa hivyo, tutashauriana na kuamua mkondo wa mambo yanayofuata,” akaongeza.

Huku familia hiyo ikilaumu serikali, Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen alifafanua tofauti kuhusu wakati Rais Ruto alihutubu na kufikishwa kwa habari kwa familia akisema polisi waliotumwa kwa familia ndio walifika bomani humo kuchelewa.

“Ilitokea kwamba wakati Rais alikuwa akihutubu, polisi hawakuwa wamefika bomani na kukutana na familia,” akasema Bw Murkomen.

“Hatimaye familia ilitembelewa na kufahamishwa kuhusu tukio hili na tutaendelea kuzungumza nao. Masuala yote na maswali waliyokuwa wakiulizia yameshughulikiwa,” akaongeza.

Waziri huyo hata hivyo hakuzungumzia kuhusu uliko mwili wa Bw Kabiru akisema habari zitatolewa katika muda ufaao.

Marehemu alikuwa katika ujumbe wa kwanza uliopelekwa kudumisha amani katika taifa hilo la visiwa vya Caribbean ambako magenge hatari yanatawala.

Naye Msemaji wa NPS, Muchiri Nyaga kupitia taarifa alisema kuwa, familia ilikuwa imefahamishwa kuhusu kutoweka kwake Machi 25.

Alitoweka kufuatia shambulizi la kushtukiza na wahuni dhidi ya msafara uliokuwa na kikosi cha Kenya.

“NPS iliwafahamisha kuhusu kutoweka kwa mwanao na imekuwa ikishauriana na kuzungumza nao. Polisi wa Haiti wamekuwa wakishirikiana na maafisa wa usalama kutoka Wakenya kumsaka. Kwenye hali ya kusikitisha, NPS imepata habari kuhusu mauti yake na familia yake imeelezwa,” akasema Bw Nyaga.

Habari za kutoweka kwa Kabiru zilifichuliwa kwa mara ya kwanza na Inspekta Jenerali wa Polisi (IG) Douglas Kanja mnamo Machi 25 mwaka huu. Tangu wakati huo, imekuwa miezi sita ya kimya cha serikali.

Jumatano, familia yake ilifika mahakamani kutaka serikali ilazimishwe kutoa taarifa kuhusu hali ya mwana wao.

Aidha, Bw Nyaga aliongeza kuwa mwili wa afisa mwingine Koplo Kennedy Mutuku Nzuve ambaye aliaga kwenye ajali Haiti, utafika nchini leo kwenye uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta.