Habari za Kitaifa

Tumerudishia Ruto pesa zake, Askofu Anyolo athibitisha

Na MERCY SIMIYU November 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KANISA Katoliki limethibitisha kwamba lilirudisha pesa ambazo lilikataa kutoka kwa  Rais William Ruto na Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja walipochangia  kanisa  la Soweto, Kayole.

Rais Ruto mnamo Novemba 17 alitoa Sh600, 000 kwa kwaya ya kanisa, Sh2 milioni kwa nyumba ya kasisi wa parokia, huku Bw Sakaja akichangia Sh200, 000. Rais Ruto aliahidi kutoa Sh3 milioni zaidi.

Siku kadhaa baadaye, Askofu Mkuu Philip Anyolo wa Dayosisi Kuu la Nairobi alitangaza katika taarifa kwamba michango hiyo itarejeshwa kwani ilikuwa kinyume na agizo la Baraza la Maaskofu wa  Katoliki Kenya (KCCB).

Sasa, Askofu Mkuu Anyolo anasema  Sh2.6 milioni kutoka kwa Rais Ruto na Sh200,000 kutoka kwa Bw Sakaja zilirejeshwa kinyume na madai ya baadhi ya wanasiasa na washirika wa kiongozi wa nchi.

Shilingi 3 milioni ambazo Rais Ruto aliahidi kwa ununuzi wa basi la kanisa hazitakubaliwa, Askofu Mkuu Anyolo alisema.

“Tumefanya tulichosema tutafanya (kurudisha michango), lakini inabakia Serikali kusema kile ambacho hatukufanya ili tukishajua kilichobaki tufanye, tuko tayari kurudisha kila kitu,” Askofu Mkuu Anyolo aliwaambia wanahabari baada ya ibada ya shukrani katika Parokia ya St Teresa, Eastleigh.

Ikulu kupitia Bw Munyori Buku, Mkuu wa Huduma za Mawasiliano ya Rais, ilisema ni Rais pekee anayeweza kuthibitisha kupokea pesa hizo.

“Huu ulikuwa mchango wa kibinafsi wa Rais kwa Kanisa. Pesa hizo hazikutolewa na Ikulu; kwa hivyo haiwezi kupokea pesa ambazo haikuchanga,” Bw Buku aliambia Taifa Leo.

Askofu Mkuu Anyolo alisisitiza kwamba michango kwa kanisa inapaswa kutolewa kwa nia njema, kwa manufaa ya wengine na sio kumdhihaki Mungu. Aliwataka watu wote, watoe kwa kanisa kwa ustawi wa jamii.

“Tunawahimiza watu wote wenye mapenzi mema kuchangia kanisa, kwani kutoa kwao kunawanufaisha wengine na kusaidia ustawi wa kijamii ya kanisa. Sio kwa kumdhihaki Mungu, bali kama tendo la kweli la shukrani na huduma,” alisema

“Tunawahimiza watu wote wenye nia njema kuchangia kanisa. Michango yao ni kwa ajili ya kuboresha wengine na ustawi wa kanisa, na si ya kumdhihaki Mungu,” aliongeza.

Askofu Mkuu Anyolo alisisitiza kwamba Kanisa litaendelea kushikilia jukumu lake kama dira ya maadili.

Hatua ya kanisa kuthibitisha  kurejeshwa kwa michango hiyo kwa Rais na Gavana Sakaja inafuatia shtuma za wabunge ambao wamewataka viongozi wa dini kuacha kujihusisha na siasa na badala yake wazingatie jukumu lao la msingi la kutoa mwongozo wa kiroho.

Wabunge hao waliwashutumu viongozi wa dini kwa kuwatwika mzigo wa  kuchangisha fedha, huku pia wakichafua sifa zao kwa kudai michango yao inatokana na rushwa.

“Lazima tupigane na ufisadi na kuhakikisha kwamba tunafanya mambo kwa uaminifu na uwazi, ninataka kuwasihi Wakenya wote kwamba tushirikiane katika kujenga taifa letu katika utawala  wa haki na uwazi katika yote tunayofanya,” alisema Askofu Mkuu Anyolo.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA