Habari za Kitaifa

Tunasubiri kufa tu, SHA haitunufaishi, wagonjwa wa saratani walilia serikali

Na MERCY CHELANGAT October 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAGONJWA wanaougua saratani wamesema kuwa sasa wamekosa matumaini ya kuishi na wanakodolewa macho na mauti huku wakilalamika kuwa Bima ya Afya ya Jamii (SHA) imekosa kugharimia matibabu yao kikamilifu.

Jana, wagonjwa wa saratani waliandamana Nairobi kuelekeza kero zao kwa SHA ambayo imekwepo kwa mwaka moja wakisema haitoshelezi matibabu yao kama Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Afya (NHIF) ambayo iliondolewa ilivyokuwa ikifanya.

Elgah Gatiri ambaye alikuwa kwenye maandamano hayo alisema anaelekea kupoteza matumaini ya kushinda vita dhidi ya saratani ya matiti ambayo alipatikana nayo Agosti 2021.

Mnamo 2022, alifanyiwa upasuaji ambapo titi lake lilikatwa na sasa amekuwa akifanyiwa tibakemia (chemotherapy) na tibaredio (radiotherapy) kuua seli za kansa zisienee zaidi.

“Tunaanza matibabu kisha yanasitishwa katikati. Ukienda Hospitali ya Kenyatta, wanakuambia bima yako imeisha na haya hutokea ukihitaji huduma za dharura na zilizomuhimu sana,” akasema.

Bi Elgar alifunguka kuwa kila sindano analodungwa baada ya kila miezi mitatu yeye hulipa Sh40,000.

Pia anameza tembe ambazo humgharimu Sh28,000 kila mwezi, pesa ambazo sasa anasema hana kabisa.

“Nimemeza tembe hizi kila siku kwa miaka miwili sasa na nimetumia pesa zangu na zote za familia yangu. Sina ajira na wao nao wamechoka na mimi, hawana pesa za kunipa tena,“SHA haifanyi kazi na nikifa leo, itakuwa kwa sababu nimekosa matibabu ya kansa kutokana na serikali hii kutomakinikia matibabu ya wagonjwa wa kansa,” akaongeza.

Kwa Agnes Waceke, hali yake inavunja moyo zaidi. Pia alipatikana na kansa ya matiti Januari mwaka huu, amefanyiwa tibakemia mara sita na pia anapaswa kudungwa sindano 18.

Alisimulia kuwa baada ya kulipia ada ya Sh6,700 ya SHA, bima hiyo iligharimia nusu ya matibabu yake pekee. Alilipa Sh6,700 nyingine na alipaswa kuendelea kudungwa sindano kama sehemu ya matibabu hayo hadi yakamilike.

“Baada ya sindano nane niliambiwa bima yangu imeisha na sasa sina pesa za kulipa. Ninahisi uchungu mwingi na siwezi lala hata nikimeza dawa za kupunguza maumivu,” akasimulia kwa masikitiko.

“Kudungwa kila sindano hugharimu Sh46,000 na bado zimebakia 10, nitapata pesa hizo wapi? Sina mume, watoto wangu wamefilisi hazina yao na sasa nimeachwa nife tu bila matibabu,” akaongeza.

Bi Waceke akidondokwa na machozi alilaani serikali na viongozi wake akisema hawajali uchungu ambao wanaougua kansa wanauhisi.

Masaibu haya hayaya kuchungulia kaburi kutokana na kansa pia yanamwaandama Margeret Wanjiru.

Bi Wanjiru amefanyiwa tibakemikali mara 15, akakatwa matiti na mnamo 2023 akaambiwa hana kansa tena baada ya kupatikana nayo 2022.

Ugonjwa huo ulirejea 2024 na kufikia mfuko wake wa uzazi kisha umeenea hadi makwapa yake.

Dawa anazotumia zinamgharimu Sh80,040 kila mwezi na itamlazimu kusubiri hadi mwaka ujao wa kifedha baada ya kuambiwa kuwa SHA haiwezi kumlipia tena.

“Maafisa wa SHA kwenye afisi zao waliniambia hawana chochote cha kufanya na lazima nisubiri hadi Februari 2026. Jinsi ninavyoendelea kukaa bila kumeza dawa na kusubiri matibabu, seli za kansa nazo zinaendelea kuongezeka na kuenea,” akasema.

“Hata familia yangu imechoka na ugonjwa huu uliofanya niwachane na mume wangu. Sina ajira, watoto wangu hawajimudu kifedha na ugonjwa huu unahitaji pesa za kuutibu ambazo sina,” akaongeza.

Wakati wa maandamano yao, waliwasilisha malalamishi yao kwa Wizara ya Afya na SHA na kusema mahangaiko ambayo wanapitia lazima yaangaziwe ili angalau waendelee na maisha yao wakipokea matibabu jinsi inavyostahili.