Habari za Kitaifa

Tunataka fidia itakayobadilisha maisha yetu, familia za waathiriwa wa maandamano zaambia kamati

Na NA WAANDISHI WETU September 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Timu ya wataalamu walioteuliwa kushughulikia fidia kwa waathiriwa wa maandamano ilianza kazi rasmi wiki hii, ambapo walipewa kionjo cha ukweli mchungu wa kazi yao baada ya mama wa mtoto wa miaka 12 aliyeuawa kwa kupigwa risasi wakati wa maandamano eneo la Rongai kutoa ombi zito kwamba “fidia hiyo iwe ya kubadili maisha.”

Bi Josinter Anyango, mama wa watoto watano kabla ya Juni 27, 2024, alimpoteza mtoto wake wa tatu, Kennedy Onyango, aliyekuwa na umri wa miaka 12 na mwanafunzi wa Darasa la Nane. Kennedy alipigwa risasi karibu na nyumba yao Rongai na video yake akiwa amelala chini, kisha kubebwa kwa pikipiki hadi hospitalini, ilisambaa sana kwenye mitandao ya kijamii na kuvunja mioyo ya wengi.

“Fidia haiwezi kumrudisha Kennedy, lakini angalau inaweza kubadilisha maisha yetu. Nilitarajia afanikiwe kimaisha na anisaidie, lakini sasa nimebaki na watoto wawili wanaougua seli mundu,” alisema Bi Anyango kwa uchungu.

Bi Anyango, anayejikimu kwa kazi ndogondogo, alisisitiza kuwa fidia pekee haitoshi – maafisa wa polisi waliowajibika lazima washtakiwe na kuadhibiwa.

“Haki kwangu ni kuona polisi aliyemuua Kennedy akikamatwa na kuhukumiwa. Si haki yeye aendelee kufanya kazi wakati sisi tunalipwa. Ni kama serikali inatuua kisha inatulipa,” alisema katika kikao kilichorekodiwa kwa video.

Timu hiyo yenye wanachama 18 iliapishwa rasmi Alhamisi iliyopita na sasa imepanga kukutana wiki hii katika Shule ya Serikali ya Kenya (KSG) ili kuandaa mpango kazi na mkakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Mwenyekiti wa timu hiyo, Profesa Makau Mutua, alisema kuwa baada ya kikao cha awali, timu itazuru maeneo mbalimbali nchini kukutana na waathiriwa moja kwa moja.

“Tutashirikiana na wananchi kote nchini. Tumeanza jana pale KICC na tutaendelea. Huu ni mchakato wa wananchi,” alisema Prof Makau.

Katika siku ya kuapishwa kwa timu hiyo, baadhi ya ndugu wa waathiriwa kama Bi Anyango walipata fursa ya kutoa ushuhuda wao. Angalau wawili walisisitiza umuhimu wa ushauri wa kisaikolojia kujumuishwa katika mchakato wa fidia.

Mmoja wao, mjane aliyepoteza mume kwa risasi, alisema mbele ya kamera:“Nilipata msongo mkubwa wa mawazo. Hadi leo nikiona mtu anashika bunduki, naona mauti. Hatukuwahi kupatiwa ushauri wowote wa kisaikolojia. Haya mateso ya kihisia bado yananisumbua. Nikipata angalau usaidizi wa ushauri, nitafurahi.”

Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo ni Rais wa Chama cha Mawakili (LSK), Bi Faith Odhiambo, ambaye alilazimika kuwahakikishia Wakenya kuwa hatavuruga kazi na yuko tayari kujiuzulu iwapo mchakato hautaendeshwa kwa uwazi na haki.

“Nikihisi juhudi zangu zimevurugwa au kudharauliwa kwa njia yoyote ile, nipo tayari kufanya jambo la heshima kwa kuzingatia sheria na Katiba ya Kenya,” alisema Bi Odhiambo.