• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 9:55 AM
Tusipolinda mazingira tunaalika umaskini, Wetang’ula aonya

Tusipolinda mazingira tunaalika umaskini, Wetang’ula aonya

NA BENSON MATHEKA

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula amesisitiza jukumu muhimu linalotekelezwa na mifumo asili katika kulinda mazingira.

Akizungumza Alhamisi, wakati wa ufunguzi rasmi wa kongamano la 27  la Maspika wa Jumuiya ya Madola (CSPOC) ambapo alitoa hotuba kuu, Spika Wetang’ula alidokeza kuwa majanga yanayohusiana na hali ya hewa yanazidi kutokea mara kwa mara na kuwa makali na kuzuia juhudi za kuangamiza umaskini barani Afrika.

Kongamano la mwaka 2024 la CSPOC lilihudhuriwa  na Rais wa Uganda Yoweri Museveni lilifanyika katika Hoteli ya Jumuiya ya Madola Munyonyo jijini Kampala, Uganda.

“Nchi za Jumuiya ya Madola, hasa zile za kusini mwa dunia, ndizo zinazokabiliwa zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa na uharibifu wa mazingira licha ya kuchangia kidogo hali hiyo,” alisema Spika Wetang’ula.

Wetang’ula alisisitiza kuwa Afrika inaathiriwa zaidi kuliko kanda nyingine na mabadiliko ya hali ya hewa licha ya mchango wa bara hilo kuwa chini ya asilimia nne ya jumla ya uzalishaji wa gesi chafu.

Spika Wetang’ula pia alieleza wasiwasi kwamba nchi za Afrika zinapaswa kutumia mapato yake katika juhudi za kukabiliana na hali hiyo, ambayo kwa sasa inakadiriwa kuwa asilimia 10 ya Pato la Taifa kila mwaka kulingana na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Akiwahutubia Maspika zaidi ya 32 kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola, alisisitiza jukumu muhimu la Mabunge akisema kuwa Bunge kama mwakilishi wa wananchi, lina jukumu kubwa la kutoa uongozi katika kukabiliana na changamoto hizi za kimataifa katika kuweka mwelekeo wa sera, kutafsiri matokeo ya michakato ya kimataifa kwa sheria za ndani; kujenga ufahamu; na  kusukuma serikali kuwajibika.

Alitoa wito kwa Mabunge ya Jumuiya ya Madola kuendelea kuwajengea uwezo wabunge katika suala la kukabiliana na tishio la mabadiliko ya tabianchi, kutenga bajeti za kutosha na kutoa fursa kwa wabunge katika ngazi ya kimataifa kubadilishana ujuzi wa jinsi ya kupunguza zaidi changamoto za kuokoa mazingira asili.

Rais Museveni alisema kuwa mkutano huo ni muhimu kwa ulimwengu kwani uliwaleta pamoja viongozi wa Mabunge ya nchi zilizo na watu 2.4  bilioni ambao ikiwa sera zinazofaa zitatekelezwa dunia itakuwa mahali pazuri pa kuishi.

Alipendekeza kuwepo kwa ushirikiano kati ya mataifa ya Kiafrika akisema kuwa maadili mema yanafaa kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika bara.

  • Tags

You can share this post!

Waathiriwa wa mafuriko wataabika baada ya kambi kufungwa

Wito jamii ya kimataifa ilazimishe kufutiliwa mbali mkataba...

T L