Habari za Kitaifa

Tutarudi barabarani Jumatatu msipoachilia Gen Z waliotekwa, vijana wa Mombasa watangaza

Na BRIAN OCHARO December 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VIJANA katika Kaunti ya Mombasa wameipa serikali muda wa saa 24 kuachilia mara moja watu wanaodaiwa kutekwa nyara na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa serikali.

Wakizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari katika ofisi za Haki Africa, vijana hao waliahidi kuungana na wenzao kote nchini kwa maandamano Jumatatu endapo madai yao hayatashughulikiwa.

Kijana na mwanaharakati wa haki za binadamu Bw Walid Sketi alisema Wakenya wamechoka na utawala wa Rais William Ruto ambao haUtaki kukosolewa.

“Serikali ya Ruto imeshindwa na kazi. Ukikosoa serikali leo na utekwe nyara kesho, basi tunajua ni nani amehusika,” alisema.

Alidai kuwa serikali inawanyamazisha wakosoaji kupitia utekwaji nyara na imeshindwa kuhakikisha haki.

 “Serikali inajua kinachoendelea. Tunasema imetosha; tumechoka na serikali isiyotaka kukosolewa,” aliongeza Bw Sketi.

 Vijana hao pia walieleza masikitiko yao kuhusu kushindwa kwa serikali kushughulikia mauaji yaliyotokea wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 mwezi Juni.

 Kwa mujibu wao, hakuna mtu yeyote aliyekamatwa au kufunguliwa mashtaka, jambo ambalo wanaamini linaashiria kufichwa kwa ukweli.

 “Hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa, hii inamaanisha serikali inajua nani alihusika na mauaji hayo,” alisisitiza Bw Sketi.

 Bi Lydia Adhiambo alilalamikia hali ya hofu na ukosefu wa usalama miongoni mwa Wakenya.

 “Tumechoshwa na utekwaji nyara na mauaji yasiyoeleweka. Leo ni Kibet; kesho inaweza kuwa mimi au wewe. Ukimya wetu utawapa watekaji nguvu zaidi,” alisema.

 Bi Adhiambo aliwataka vijana kuwa macho, akisema kwamba utekwaji nyara umewanyima Wakenya amani na utulivu.

 “Tunapaswa kuwa na familia zetu sasa, lakini badala yake tuko hapa kwa sababu ya utekwaji nyara. Tunaishi kwa hofu, tukitazama nyuma kila mara. Wauaji wanaachiwa huru ilhali Wakenya wasio na hatia wanatekwa nyara,” alilalamika.

Hata hivyo, vijana hao walitoa dai thabiti, wakisema kuwa utekwaji nyara na vitisho vya mara kwa mara kwa maisha yao havitawazuia kudai utawala bora na pia heshima kwa haki za binadamu.

 “Serikali lazima ichukue hatua ndani ya saa 24. La sivyo, tutarudi barabarani,” alionya Bi Adhiambo.

 Vijana hao pia wamemtaka aliyekuwa  Naibu Rais Rigathi Gachagua kutoa maelezo kamili kuhusu kikosi cha utekwaji nyara alichokitaja siku ya Ijumaa.

 Bw Gachagua alidai kuwa kikosi hicho kinafanya kazi nje ya mamlaka ya Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na kinaongozwa na moja ya  jamaa za afisa mkuu  serikalini.

 Hata hivyo, vijana hao wanamtaka Bw Gachagwa kutoa maelezo zaidi kuhusu watu hao na mahali wanaotekwa nyara wanazuiliwa.

 “Bw Gachagua asitupatie habari nusu. Lazima ataje watekaji, maafisa wakuu waliohusika, na maeneo maalum watekwa nyara wanateswa au  anyamaze,” alisema Bi Adhiambo.

 Mbali na madai yao, vijana hao walimlaumu Rais Ruto kwa kutumia dini kukandamiza wakenya

 “Vitabu vitakatifu kama Bibilia vinapinga vikali kile Rais Ruto anachofanya. Anadai kutokujua kuhusu utekwaji nyara, lakini kila kitu kiko wazi,” walisema.

 Vijana hao pia wamemkashifu Bw Kanja  na kumtaka ajiuzulu wakisema ameshindwa na kazi aliyoajiriwa kufanya.

 Bi Christine Khabuya  alimkosoa Bw Kanja kwa kushindwa kushughulikia suala la utekaji nyara wa vijana nchini.

“Kama Bw Kanja hajui ni nani anayewateka nyara Wakenya, basi anapaswa kujiuzulu. Kazi yake ni ipi ikiwa hajui masuala nyeti kama haya ya usalama?” alihoji.

Wale wanaodaiwa kutekwa nyara ni pamoja na Karani Mwema, Rony Kiplagat, Martin Mwau, Billy Munyiri, Peter Njeru, mchora katuni Gideon Kibet (“Kibet Bull”), na Bernard Kavuli.

Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu nchini (KNCHR) imeripoti visa 82 vya utekwaji nyara tangu Juni 2024, huku watu 29 wakiwa bado hawajapatikana.