Habari za Kitaifa

Tutawaongezea mishahara mwaka huu, Gachagua ahakikishia polisi

January 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na JAMES MURIMI

SERIKALI imewahakikishia maafisa wa Huduma ya Polisi nchini (NPS), Huduma ya Magereza na Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) kwamba nyongeza ya mishahara yao ya asilimia 40 itaanza kutekelezwa Julai mwaka huu.

Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto, imejitolea kutekeleza mapendekezo ya ripoti ya mageuzi ya polisi yaliyokusanywa na jopokazi lililoongozwa na aliyekuwa jaji mkuu David Maraga.

“Kuanzia Julai 1 mwaka huu, tutaanza kuongeza mishahara ya walinzi wetu wa magereza katika muda wa miaka mitatu kwa asilimia 40.

“Motisha ya maafisa wetu itakapoimarishwa, wataweza kuwachunga vyema wafungwa,” alisema Bw Gachagua, Jumatatu alipowatembelea wafungwa katika Gereza Kuu la King’ong’o.

“Jinsi mnavyofahamu, Rais wetu alipokea mapendekezo kutoka kwa Maraga. Ningependa kuwahakikishia maafisa wa magereza kuwa nyongeza ya mishahara yao itaanza mara moja kuanzia Julai,” alisema.

Bw Gachagua na mke wake Pasta Dorcas Rigathi walijiunga na wafungwa kusherehekea Mwaka Mpya kwenye hafla iliyoitwa “Ibada na Karamu ya Mwaka Mpya Jela ya King’ong’o”.

“Rais William Ruto na naibu wake wanajitahidi kuhakikisha vituo vyote vya kurekebisha tabia nchini vina mazingira mwafaka ili kuwatoa raia waliorekebisha tabia,” alisema Bi Dorcas.

Hii ni jela ya nne ambayo Pasta Dorcas amezuru katika kufanikisha shabaha yake kuhusu “mustakabali wenye hadhi kwa Wanajamii Waliotengwa” ikiwemo watoto wavulana na wanaume nchini.