Habari za Kitaifa

Uasin Gishu, Baringo na Elgeyo Marakwet makao makuu ya ufisadi nchini – Ripoti

Na ERIC MATARA August 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KAUNTI za Uasin Gishu, Baringo na Elgeyo Marakwet ni miongoni mwa kaunti zilizo na kiwango cha juu cha ufisadi nchini, huku wanaotafuta huduma katika kaunti hizo wakilazimika kutoa hongo ili kuhudumiwa.

Kaunti nyingine katika kumi-bora kwa ufisadi zinajumuisha Marsabit, Embu, Homa Bay, Bomet, Kakamega, Tana River, Kiambu, Meru, Nyamira na Wajir.

Pia Kwale, Kilifi, Mandera, Tharaka Nithi, Kitui, Murang’a, Samburu na Vihiga zimetajwa kuwa na viwango vya juu vya ulaji rushwa.

Hii ni kulingana na ripoti mpya iliyotolewa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) jana, kuhusu hali ya hongo nchini.

Kwa mujibu wa Utafiti wa Kitaifa kuhusu Maadili na hali ya Ufisadi (NECS) 2024, kaunti za Elgeyo Marakwet, Marsabit na Wajir zinaongoza kwa visa vya wakazi kutakiwa kutoa hongo wakitafuta huduma.

EACC inasema kuwa kila wakati wakazi wanapohitaji huduma katika kaunti hizi, kuna uwezekano mkubwa wa mtu kuombwa kutoa hongo.

“Elgeyo Marakwet, Marsabit na Wajir ni kaunti ambazo hongo ilihusishwa kwa kiwango cha juu sana, ambapo asilimia 100 ya walioomba huduma walilazimika kutoa hongo,” inasema sehemu ya ripoti hiyo ya EACC.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa utoaji wa hongo ulikuwa na mafanikio zaidi katika kaunti za Kakamega, Baringo na Meru.

Kila mara mtu alipotoa hongo katika kaunti hizo, alijiweka katika nafasi nzuri ya kupata huduma kwa asilimia 1.37 ikilinganishwa na wale ambao hawakutoa hongo.

Kwa wastani, kaunti zilizoathirika zaidi na vitendo vya utoaji hongo ni Uasin Gishu, Baringo, Embu, Homa Bay, Bomet, Kakamega, Tana River, Kiambu, Nyamira na Wajir.

“Kwa wastani, kiasi kikubwa zaidi cha hongo kiliripotiwa katika kaunti ya Uasin Gishu (Sh25,873), ikifuatiwa na Baringo (Sh16,156), Embu (Sh12,878), Homa Bay (Sh12,381), Bomet (Sh11,650), Kakamega (Sh10,013), Tana River (Sh9,582), Kiambu (Sh7,982), Nyamira (Sh7,748) na Wajir (Sh7,275),” inaongeza ripoti hiyo.

Kiwango cha juu cha hongo kitaifa kililipwa Uasin Gishu (asilimia 11.12), ikifuatiwa na Baringo (asilimia 6.94), Embu (asilimia 5.54), Homa Bay (asilimia 5.32) na Bomet (asilimia 01).

Hii inaashiria kuwa wanaotafuta huduma katika kaunti hizo wana uwezekano mkubwa wa kuombwa hongo ili wahudumiwe.

Kwa mfano, kila wakati mtu akitafuta huduma katika kaunti za Kwale, Kilifi na Wajir, ana uwezekano wa kuombwa hongo kwa asilimia 1.09, 1.03 na 1.02, mtawalia.

Kaunti nyingine ambazo kuna uwezekano wa kuombwa hongo kwa kiwango cha asilimia 1.00 ni Mandera, Marsabit, Tharaka Nithi, Kitui, Murang’a, Samburu, Elgeyo Marakwet, Vihiga, Homa Bay na Nyamira.

Huduma nyingi za umma ambapo utoaji wa hongo ni wa kawaida zaidi ni pamoja na za ardhi na makazi ya kaunti, ukaguzi na usimamizi, malipo kutoka kwa serikali ya kaunti, ujenzi wa miundomsingi ya maji na usafi wa mazingira, huduma za afya, leseni za kaunti, miongoni mwa nyingine.

Bodi za Utumishi wa Umma katika kaunti pia ni miongoni mwa taasisi zilizojaa visa vya hongo.

Kwa wastani, walioshiriki utafiti walisema walitoa kiasi kikubwa cha hongo walipotafuta ajira kutoka kwa serikali za kaunti, ambapo walitoa Sh243,651 kwa wastani.

Ripoti hiyo ya EACC imeonyesha kuwa kila mara mtu alipotoa hongo katika taasisi hizo, alikuwa na uwezekano mara mbili zaidi wa kupata huduma ikilinganishwa na wale ambao hawakutoa hongo.

Kwa upande mwingine, kaunti ambazo mtu alikuwa na uwezekano mdogo wa kuombwa hongo ni Nakuru, Makueni, Kajiado, Narok, Siaya, Kisumu, Trans Nzoia, Nyeri, Bungoma, Lamu, Nyandarua na zingine.

Asilimia kubwa ya washiriki (43) walitoa hongo kwa sababu waliambiwa “ni lazima”, wakifuatiwa na asilimia 23.3 waliodai kuwa ilikuwa njia pekee ya kupata huduma, na asilimia 18 walitoa hongo ili kuepuka kucheleweshwa kwa huduma.

Hata hivyo, la kushangaza ni kwamba ripoti imefichua kuwa asilimia 92 ya waathiriwa wa visa vya hongo hawakuripoti kwa mamlaka yoyote. Ni asilimia 2.8 pekee walioripoti rasmi.

NECS 2024 ililenga familia 6,000, lakini jumla ya familia 5,960 ndizo zilizohojiwa kutoka kaunti zote 47 nchini.
Utafiti ulifanyika kuanzia Novemba 6 hadi Desemba 1, 2024.

Ripoti hiyo ililenga kubaini idara za serikali za kaunti na taifa zinazotajwa kuwa na ufisadi na maadili ya kiwango duni.

Utafiti huo pia umeonyesha kuwa washiriki wengi walikuwa na imani kubwa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika vita dhidi ya ufisadi.

Katika ripoti ya NECS 2024, zaidi ya asilimia 60 ya washiriki walisema hawaridhishwi na viwango vya uadilifu, uwazi na uwajibikaji katika utoaji huduma za umma katika kaunti.

Tafsiri: BENSON MATHEKA