Ubomoaji wa jengo hatari wasababisha Hospitali Kuu ya Pwani kubaki mahame wagonjwa wakihamishwa
HOSPITALI kuu ya rufaa eneo la Pwani iliyojengwa wakati wa ukoloni, mwaka 1908, ilifungwa kwa mara ya kwanza na kusalia mahame baada ya wagonjwa 519 kuondolewa.
Wagonjwa hao pamoja na wale waliokuwa hali mahututi walipelekwa katika hospitali mbalimbali ikiwemo Tudor, Port Reitz na Utange huku wale waliokuwa mahututi wakipata nafasi katika hospitali ya kibinafsi ya Pandya.
Wagonjwa hao walihamishwa kutoka hospitali hiyo ili wasipate mshtuko wa moyo wakati wanajeshi walipokuwa wakibomoa jengo la ghorofa 11 wakitumia vilipuzi.
Hata hivyo, mgonjwa mmoja aliaga dunia wakati wa kuhamishwa.
Afisa mkuu wa hospitali hiyo Dkt Iqbal Khandwalla alipinga madai kwamba mgonjwa huyo aliaga dunia sababu ya kuhamishwa, akisisitiza alikuwa katika hali mahututi.
“Alikuwa mahututi, hakuaga dunia kwa sababu ya kuhamishwa. Tuliweza kuhamisha wagonjwa wote salama na wale waliokuwa na nafuu wakiruhusiwa kwenda nyumbani. Takriban wagonjwa 282 walipelekwa hospitali mbalimbali kuendelea na matibabu,” alisema Dkt Khandwalla.
Gavana wa Mombasa Bw Abdulswamad Nassir alisema kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa huduma za afya katika hospitali hiyo ililazimika kufungwa na wagonjwa hata wale waliokuwa kwenye vyumba vya mahututi kuhamishwa ili kuokoa maisha yao.
Alisema hospitali hiyo itasafishwa na kupuliziwa dawa maalum kabla ya kufunguliwa kuanzia Ijumaa, Aprili 11, 2025.
“Lazima tujitayarisha vilivyo kabla ya kuruhusu wagonjwa warejee,” alisema Bw Nassir.