Uchunguzi: Masomo bora Kenya sasa ni ya matajiri
NA DAVID MUCHUNGUH
WAKENYA wanatumia mabilioni ya fedha kugharamia elimu ya watoto wao katika shule za kibinafsi kutokana na kushuka kwa viwango vya mafunzo yanayotolewa katika shule za umma.
Hii ni licha ya kwamba wao hulipa viwango vya juu vya ushuru kugharamia elimu ya msingi, kulingana na matokeo ya utafiti ulioendeshwa na Taifa Leo.
Uchunguzi wetu pia umebaini kuwa serikali ya sasa na zile za zamani zilifeli kuoanisha ongezeko la wanafunzi na miundo msingi ya shule.
Hali hiyo imechangia misongamano katika shule za umma hali inayoshusha viwango vya elimu.
Wazazi na wadau waliozungumza na Taifa Leo walisema masomo yanaendelea kubinafsishwa “kwa lazima” haswa katika viwango vya chechekea (ECDE) na shule za msingi.
Maswali sasa yanaibuliwa kuhusu matumizi ya fedha za sekta ya elimu iliyotengewa zaidi ya Sh668 bilioni katika bajeti ya kitaifa ya mwaka huu ikiwa sawa na asilimia 30 ya bajeti.
Ajabu ni kuwa kiasi kamili cha fedha zilizotengwa katika bajeti huwa hakifikii shule kwani zinadai malimbikizi ya Sh54 bilioni, kutoka kwa serikali, kama mgao kwa shule.
Familia zinazoishi katika maeneo ya miji zinaathiriwa zaidi kutokana na uhaba wa shule za umma ambako watoto wao wanaweza kusomea.
Hii imewalazimu kupeleka watoto wao, waliofikisha umri wa kwenda shule, katika shule za kibinafsi kwa gharama kubwa.
Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amekubali kuwa karibu asilimia 70 ya watoto katika Kaunti ya Nairobi husomea shule za kibinafsi.
Aliongeza kuwa kati ya watahiniwa 48, 000 waliopata gredi ya E katika mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) wa 2023, wanafunzi 10, 000 kati yao wanatoka Nairobi.
Bw Machogu alisema uwekezaji finyu katika ujenzi wa shule za umma jijini Nairobi umechangia uhaba wa shule.
Wawekezaji wa kibinafsi wamejitokeza kujaza pengo hilo.
Waziri Machogu alisema afisi yake na ile ya elimu katika Kaunti ya Nairobi zitabuni jopokazi maalum kukagua shule kubaini ikiwa zinaafiki mwongozo uliowekwa na Wizara ya Elimu wa kuanzisha shule.
“Tunakabiliwa na hali mbaya zaidi Nairobi; hatua inapasa kuchukuliwa kurekebisha hali. Tutashirikiana na serikali ya kaunti kutambua ardhi ya umma ya kujenga shule za umma.
Aidha, tutasaka usaidizi kutoka kwa sekta ya kibinafsi kufanikisha azma hii,” Bw Machogu akaambia Taifa Leo.
Kulingana na data kutoka kwa Wizara ya Elimu, kuna shule 216 za chekechea, shule 211 za msingi, shule 193 za upili ya msingi na shule 107 za upili za umma katika Kaunti ya Nairobi, zinazohudumia watu milioni tano.
Aidha, kuna shule za chekechea 952, shule 780 za msingi, shule 672 za upili za msingi na shule 207 za upili za kibinafsi katika Kaunti ya Nairobi.
Hii inaonyesha kuwa karibu asilimia 71 ya shule katika jiji kuu nchini Kenya zinamilikiwa na watu au mashirika ya kibinafsi.
Hii ni kinyume na wajibu wa serikali wa kutoa elimu ya msingi ya lazima na isiyolipiwa kwa watoto wote nchini.