Habari za Kitaifa

UDA haitaachia ODM kiti chochote chaguzi ndogo za Novemba, Katibu Hassan Omar asema

Na WINNIE ATIENO August 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto na Kinara wa ODM wanakabiliwa na mtihani kwenye ndoa yao ya kisiasa baada ya chama cha UDA anachokiongoza Kiongozi wa Nchi kusema kuwa kitawasimamisha wagombeaji katika viti vyote kwenye chaguzi ndogo zitakazoandaliwa mnamo Novemba.

Mnamo Novemba 27, 2025, wagombea wa viti vya uwakilishi wa wadi, ubunge na useneta kutoka vyama mbalimbali watamenyana.

Jumla ya viti vyote vitakavyogombewa ni 23.

Chama cha UDA kimeanza kuweka mipango ili kuhakikisha kinanyakua viti vingi kwenye chaguzi hizo. Hii leo wagombea wa UDA watakutana na wakuu wa chama hicho kujadili kuhusu chaguzi hizo.

“Sitaki kufichua mipango yetu kabla mkutano maalum lakini tutahakikisha demokrasia inazingatiwa,” akasema Katibu Mkuu wa UDA, Hassan Omar.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, akiwa Mombasa, Bw Omar alifichua kuwa chama cha Rais Ruto kitakuwa na wagombea katika viti vyote vya kisiasa kwenye chaguzi hizo ndogo.

“UDA imejitayarisha kwa chaguzi ndogo za Novemba, ndiyo maana Ijumaa iliyopita tulichapisha tangazo tukialika wagombea wetu wote walio na nia ya kuombea viti hivyo kujitokeza kwa mkutano kujadili masuala hayo,” alisema Bw Omar.

Bw Omar alisema ipo haja ya kuhakikisha kuna demokrasia katika vyama vya kisiasa.

Mwanasiasa huyo alisema kutakuwa na makubaliano kati ya vyama vya kisiasa vilivyo kwenye muungano wa serikali ya Kenya Kwanza.

Hata hivyo, alisema lazima UDA ipewe kipaumbele kwenye maongezi yoyote ya kinyang’anyiro hicho.

“UDA itanyakua viti vingi sana. Tuna matumaini sababu tumefanya kazi mashinani na tuna wagombea wetu. Kuna mapatano kati ya Rais Ruto na Bw Odinga na walikubaliana mambo mengi sana likiwemo suala la uchaguzi mkuu ujao,” aliongeza.

Alisema chama hicho kitasimamisha wagombea Kasipul-Kabondo, Magarini, Ugunja, Baringo (seneta), Mbeere North, Malava, Banisa na viti vya uwakilishi wadi.

“Hatutaki kuwe na dhana kwamba tumegawa viti hivi. UDA ni chama cha kitaifa na viongozi wetu wanatoka sehemu zote nchini. Kwa hivyo, kuna haki na uhuru wakimenyana na wenzao debeni,” alisema Bw Omar.

Haya yanajiri huku ODM ikiendelea kushinikiza UDA isisimamishe mgombea katika kiti cha Magarini.

Viongozi wa Kilifi wakiongozwa na Gavana Gideon Mung’aro, Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Kilifi, Bi Getrude Mbeyu, Wabunge Amina Mnyazi (Malindi), Bw Peter Kanata (Kaloleni), Seneta Bw Stewart Mwadzaya wamekuwa wakishinikiza Rais Ruto na Bw Odinga wampe tikiti aliyekuwa mbunge wa Magarini Harrison Kombe na aungwe pia na Kenya Kwanza.

Bw Kombe alipoteza kiti hicho Mei mwaka jana baada ya Mahakama ya Juu kudumisha uamuzi wa Mahakama Kuu kwamba kulikuwa na udanganyifu na wizi wa kura katika uchaguzi uliopita.

Mahakama ya Juu ilishikilia ya kwamba mbunge huyo wa chama cha ODM alipoteza kiti chake cha ubunge hivyo basi wananachi warudi debeni.

“Bw Kenga atakuwa debeni kupitia tikiti ya UDA, hatutakuwa na mchujo. Lazima tuhakikishe usawa na haki. Bw Kenga alienda mahakamani na uamuzi ukatoka. Kama Bw Kombe ni maarufu wakutane debeni na mgombea wetu,” alisema Bw Omar.