Habari za Kitaifa

UDA, ODM warukana kuhusu kuachiana viti 2027 ndoa ikizidi kufifia

December 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VYAMA vya kisiasa vimeanza kupanga mikakati yao binafsi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027 baada ya chaguzi ndogo zenye ushindani mkali zilizohusisha mazungumzo na makubaliano ya kugawana baadhi ya maeneo yenye ushindani.

Chama cha United Democratic Alliance (UDA) sasa kimesema hakitaruhusu tena mpango wa kugawana maeneo na vyama vingine tanzu vya Kenya Kwanza au chama cha ODM, ambacho kwa sasa ni sehemu ya serikali jumuishi, katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Katibu Mkuu wa UDA, Hassan Omar, alisema mpango wa kugawana maeneo ulihusu chaguzi ndogo pekee na kwamba chama kitawasilisha wagombeaji kote nchini ifikapo 2027.

Alisema uchaguzi wa ndani wa chama uliopangwa Januari 10, 2026 utasaidia kukijenga katika ngazi za mashinani.

“Tayari tumetambua wagombeaji watakaopata tiketi za moja kwa moja kwa kuwa ni nguzo thabiti ndani ya chama. Kwa mfano, Kaunti ya Kilifi UDA itamsimamisha Jimmy Kahindi kwa ugavana baada ya aliyekuwa waziri wa serikali Aisha Jumwa wiki iliyopita kutangaza kujiondoa kutoka chama tawala,” alisema Bw Omar.

Bi Jumwa alihamia chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kinachoongozwa na Spika wa Seneti, Amason Kingi, ambacho alikitaja kuwa ‘cha nyumbani’.

Alisema alifanya mashauriano ya kina na uongozi na wafuasi wake kabla ya kujiunga na PAA.

Katika uchaguzi mdogo wa Novemba 27, vyama tanzu vya Kenya Kwanza vilijiondoa katika kinyang’anyiro cha ubunge Magarini na kumuunga mkono mgombea wa ODM, Harrison Kombe.

Aliyekuwa mgombeaji wa UDA, Stanley Kenga, alikihama chama hicho na kujiunga na Democracy for Citizens Party (DCP)akipinga hatua hiyo.

UDA pia haikusimamisha wagombeaji katika maeneo kadhaa yanayochukuliwa kuwa ngome za ODM Nyanza, ikiwemo Ugunja na Kasipul.

Vivyo hivyo, ODM haikusimamisha wagombeaji kwa uchaguzi mdogo wa Seneta Baringo na ubunge Mbeere Kaskazini miongoni mwa maeneo mengine.

Baadhi ya wagombea wa vyama tanzu vya Kenya Kwanza waliolazimika kujiondoa walizawadiwa nyadhifa za serikali. Wakati wa kampeni Magarini, ilibainika kuwa Bw Kenga alikataa kazi serikalini.

Mabadiliko ya hivi karibuni ya uaminifu wa kisiasa Kilifi, yanaashiria hatua pana ya vyama kujitenga na makubaliano ya kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2022 kuelekea uchaguzi ujao.

Kwa kawaida, vyama hunufaika zaidi katika miungano kulingana na nguvu wanazoleta mezani, na ushirikiano wa ODM na UDA umeathiri vibaya vyama vidogo vilivyonufaika chini ya Kenya Kwanza mwaka 2022.

Kiongozi wa ODM, Dkt Oburu Oginga, alisema licha ya wagombeaji wa serikali jumuishi kushinda viti vyote katika chaguzi ndogo, chama kinapaswa kuimarishwa.

“Chama chetu ODM lazima kiwe imara. ODM ni chama cha kitaifa, si cha eneo fulani,” alisema.

Akizungumza Nairobi katika hafla ya kuwapongeza wanachama wa ODM walioshinda kwenye chaguzi ndogo, Seneta huyo wa Siaya, alisema wanakusudia kusimamisha wagombea kote nchini mwaka 2027.

Alisisitiza kuwa serikali jumuishi ni mpango maalum uliolengwa kudumu hadi 2027.

“Ikiwa hatutafanya kazi kwa bidii na kukiimarisha chama, tutajikuta tukiachwa nyuma. Sisi ni chama chenye maono na tunataka kuendelea kuwahudumia wananchi.

Mpango wa serikali jumuishi una ajenda 10 tunazotaka zitekelezwe kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027,” alisema.