Habari za Kitaifa

UDA yamalizana na Orwoba IEBC ikijaza nafasi yake katika Seneti

Na JUSTUS OCHIENG’ August 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imemteua rasmi Bi Consolata Nabwire Wakwabubi kuchukua nafasi ya Gloria Orwoba kama Seneta Mteule wa Chama cha UDA, kufuatia kufukuzwa kwa Bi Orwoba kutoka chama hicho.

Katika tangazo maalum la gazeti rasmi la serikali lililochapishwa Ijumaa, Agosti 15, Mwenyekiti wa IEBC Bw Erastus Ethekon alieleza kuwa Bi Wakwabubi atachukua nafasi ya uwakilishi wa wanawake kupitia uteuzi wa UDA katika Seneti.

Uamuzi huo umetokana na kufutwa kwa jina la Gloria Orwoba kutoka sajili ya wanachama wa UDA, jambo lililosababisha kupoteza moja kwa moja kiti chake cha Seneta Mteule.

“Kulingana na Kifungu cha 37 cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2011, na baada ya kufutwa kwa Gloria Magoma Orwoba kutoka sajili ya wanachama wa UDA, Tume inarekebisha Tangazo la Gazeti Na. 10537 la mwaka 2022 na kuingiza jina la Consolata Nabwire Wakwabubi,” linasema tangazo hilo kwa sehemu.

Katiba ya Kenya kupitia Kifungu cha 90 na Sheria ya Uchaguzi, inapatia IEBC mamlaka ya kugawa upya viti vya uteuzi wa vyama iwapo mwanachama aliyeteuliwa atapoteza uanachama wa chama kilichomuidhinisha.

Sheria inasema kuwaanayefuata kwenye orodha ya chama iliyowasilishwa kabla ya uchaguzi mkuu, ndiye anayechukua nafasi hiyo iliyoachwa wazi..

Bi Orwoba aliteuliwa Seneta  Septemba 2022 kupitia tiketi ya UDA lakini muda wake ulikumbwa na mivutano ya ndani ya chama. Baraza  Kuu ya UDA (NEC) ilipitisha uamuzi wa kumfukuza kwa madai ya utovu wa nidhamu na kuvunja kanuni za chama.

Uamuzi huo ulithibitishwa na Mahakama ya Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa pamoja na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa, hivyo kuipa IEBC nafasi ya kuteua mrithi wake.