Habari za Kitaifa

Ufanisi wa washirika uchaguzini wampa Ruto kizungumkuti cha naibu wa rais 2027

Na MWANGI MUIRURI December 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto sasa anakabiliwa na kibarua kigumu cha kumteua mgombea mwenza wake katika uchaguzi mkuu wa 2027 baada ya Prof Kithure Kindiki kuonyesha ukakamavu wake kwa kushindia UDA kiti cha Mbeere Kaskazini.

Mjadala kuhusu mgombea mwenza wa Rais Ruto umekuwa gumzo kwa muda sasa huku suala kuu likiwa iwapo Prof Kindiki ataweza kumsaidia kudumisha umaarufu wake katika ukanda wa Mlima Kenya au la.

Naibu wa Rais na Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku walikuwa uso wa kampeni za mgombeaji wa UDA, Leo Muthende aliyekitwaa kiti hicho kwenye uchaguzi mdogo ulioandaliwa Alhamisi.

Mbali na Prof Kindiki, viongozi wengine wanaopigiwa upatu kuwa mgombea-mwenza wa Rais 2027 ni Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Gavana wa Homa Bay ambaye pia ni Mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga.

Bw Mudavadi na Bi Wanga pia walitia fora kwenye chaguzi ndogo ambazo ziliandaliwa wiki jana. Bi Wanga aliongoza ODM kutwaa viti vya ubunge vya Kasipul na Ugunja katika eneo la Luo Nyanza.

Pia ODM ilifaulu eneo la Pwani ambapo Harrison Kombe alishinda ubunge wa Magarini, Kilifi.

Mawimbi ya kisiasa ya Bw Mudavadi yalikuwa makali huku akihimili ushindani mkali eneo la Malava na kuhakikisha David Athman Ndakwa wa UDA anambwaga Seth Panyako wa DAP-K.

Kwa mujibu Mchanganuzi wa Kisiasa Phillip Kisia, kubadilika kwa ramani ya kisiasa kunaendelea kuvuruga mipango na mikakati ya Rais ya 2027.

Bw Kisia ambaye pia ni mwanasiasa jijini Nairobi, anasema anatarajia kuwa Rais atafanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri.

“Ni wazi kuwa Rais sasa lazima acheze karata zake vizuri hasa kuhusu hili suala la mgombea-mwenza. Lazima awe makini kuhusu takwimu kisha atathmini idadi ya kura ambazo kila anayemezea wadhifa huo atamletea,” akasema Bw Kisia.

Kwa sasa kuna uhasama ambao unatokota ndani kwa ndani kati ya kambi ya Prof Kindiki na wanasiasa wa ODM.

Baadhi ya wanasiasa wa ODM wamezua maswali kuhusu uwezo wa Prof Kindiki kumsaidia Rais kupata asilimia 87 ya kura alizopata Mlima Kenya mnamo 2022.

Wanasiasa wa ODM na baadhi ya viongozi kutoka Magharibi nao wanahoji nafasi yao serikalini iwapo Prof Kindiki ataidhinishwa kuwa mgombea mwenza wa rais 2027.

Viongozi wa ODM Nyanza na Magharibi wamekuwa wakitaka wadhifa huo.

Kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga kwenye mahojiano na Taifa Leo mwezi uliopita alisema chama hicho kitaingia kwenye muungano wowote wa kisiasa ambapo kitahakikishiwa urais au mambo yakienda vibaya sana basi naibu rais.

Prof Peter Kagwanja, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa anasema kauli ya Dkt Oginga ni mbinu ya kuhakikisha uungwaji wa ODM kwa Rais Ruto usichukuliwe kama jambo la kawaida na hakikisho.

“Mbali na kutaka wadhifa wa naibu rais, ukitathmini kauli ya Dkt Oginga, anataka ODM itunukiwe nyadhifa zaidi sasa kabla ya kuanza kuzungumzia suala la 2027,” akasema Prof Kagwanja.

Naye Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa Festus Wangwe anasema chaguzi hizi ndogo zimefanya rais ajikune kichwa zaidi kwa sababu mirengo yote inayomezea mate unaibu rais ilipata ushindi.

“Rais amechanganyikiwa zaidi kwa sababu washirika wake wote walipata ushindi. Sasa lazima atafakari zaidi kwa sababu wote wameonyesha wanaweza kumsaidia kupata kura,” akasema Bw Wangwe.

Bw Wangwe anatabiri kuwa mgombea-mwenza wa rais 2027 atatoka Mlima Kenya, Nyanza, Ukambani au Magharibi.

“Prof Kindiki, Anne Waiguru, Cecily Mbarire, Mwangi Kiunjuri, Ndindi Nyoro au Irungu Kang’ata wanaweza kuwa mgombea-mwenza 2027 kutoka Mlima Kenya,” akaongeza.

Kutoka Magharibi anamtaja Bw Mudavadi, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangúla, Gavana George Natembeya na Katibu wa ODM, Edwin Sifuna.

Ukambani kuna Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka na Dkt Alfred Mutua.

Nyanza ambako ODM inatamba, Rais anaweza kumteua Bi Wanga, Winnie Odinga ambaye ni mwanawe Raila na mbunge wa EALA, na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino.