Habari za Kitaifa

Ufichuzi: Jinsi familia ya Kenyatta inavuna mabilioni kupitia dili ya Expressway

Na BRIAN WASUNA July 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

FAMILIA ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta sasa imehusishwa na sakata ya ufisadi kuhusiana na mradi wa ujenzi wa barabara ya moja kwa moja ya Nairobi Expressway mnamo 2021.

Kesi iliyoko mbele ya Jopo la Kutatua mizozo kuhusu Ushuru inaweka wazi jinsi kampuni zinazomilikiwa na washirika wa familia hiyo zilipewa zabuni za mabilioni ya fedha katika mradi huo.

Moja ya kati ya kampuni ni Edge Worth Property inayomilikiwa na Rose Wamaitha Ng’ote.

Mnamo Machi 26, 2021 kampuni hiyo ilirithi hisa zote za kampuni ya Ropat Trust Company Ltd.

Muda mfupi baadaye, Edge Worth Properties Ltd ilitoa ardhi yake kwa kampuni ya Cale Infrastructure Construction Company Ltd, mwanakandarasi mkuu wa ujenzi wa Nairobi Expressway, kwa uchimbaji wa mchanga wa kutumika katika mradi huo.

Cale Infrastructure pia ilitarajia kutumia ardhi hiyo kama eneo la kuhifadhi vifaa vya ujenzi.

Kampuni hiyo ilipewa kandarasi hiyo chini ya mpango wa ushirikiano kati ya serikali na kampuni ya kibinafsi (PPP) ambapo iliwekeza Sh88 bilioni kwa ujenzi wa barabara hiyo ya umbali wa kilomita 27.1.

Baadaye ingerejesha pesa zake kwa kudai ada kutoka kwa watumiaji wa barabara hiyo.

Mzozo wa ushuru sasa umefichua kuwa Bi Ng’ote na Ropat Trust walikuwa vibaraka wa familia ya Kenyatta.

Kinaya ni kwamba ni wakati huo, 2021 ambapo Bw Kenyatta alikuwa akipinga vikali mtindo wa maafisa wa serikali na watu wa familia zao kujitajirisha kwa kufanya biashara na serikali.

Ili kuonyesha kujitolea kwake kuzima uovu huo, Bw Kenyatta alimwagiza aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Paul Kihara Kariuki kuandaa Mswada wa Dhidi ya Mgongano wa Kimasilahi (Conflict of Interest Bill) akilenga kuitumia kuwazuia watumishi wa umma kufanya biashara na serikali.

Taifa Leo haikubaini kiasi cha pesa ambazo familia ya Kenyatta ilipata kutokana na sakata hiyo ya mchanga.

Lakini kesi iliyoko katika Jopo la Kutatua Mizozo kuhusu Ushuru inaonyesha kuwa katika mwaka wa 2022 pekee, kampuni ya Edge Worth Properties ililipa mgao wa faida (dividends) wa Sh1 bilioni kwa mwanahisa wake wa kipekee, Enke Investment.

Kwa kuwa kampuni hutenga kati ya asilimia 35 na 55 ya faida yake kwa malipo ya “dividends” hii ina maana kuwa huenda Edge Worth Properties iliingiza mapato ya kati ya Sh1.8 bilioni na Sh2.8 bilioni mnamo 2022 pekee.

Msemaji wa Bw Kenyatta Kanze Dena Mararo hakujibu maswali yetu kuhusu uwezekano wa uwepo wa mgongano wa kimasilahi katika biashara kati ya kampuni za Edge Worth Properties na Cale Infrastructure.

Hii ni hata baada ya sisi kufuatilia suala hilo kwa muda wa wiki mbili zilizopita.

Kampuni ya Cale Infrastructure pia haikujibu maswali yetu kuhusu jinsi ilifikia uamuzi wa kuipa kampuni ya Edge Worth Properties zabuni ya kuipa mchanga wa ujenzi.

Kampuni ya Enke Investments ilisajiliwa mnamo Aprili 26, 1989 na inamilikiwa na familia ya Kenyatta.

Aliyekuwa Mama wa Taifa Mama Ngina Kenyatta, mwanawe Muhoho Kenyatta na kampuni ya Goodison Trust Corporation wameorodhesha kama wamiliki wa kampuni hiyo, Enke Investment Ltd, kila mmoja akimiliki hisa 1.333 milioni.

Mkewe Uhuru, Margaret Kenyatta anamiliki hisa mbili katika kampuni ya Goodison Trust Corporation.

-IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA

Habari kwa Kiingereza: Tax row exposes Kenyatta family expressway deal