UFICHUZI: Ruto anajenga kanisa la Sh1.2 bilioni Ikulu
RAIS William Ruto kwa siri anajenga kanisa kubwa ndani ya uwanja wa Ikulu ya Nairobi, hatua ambayo inazua maswali kuhusu suala la kutenganisha dini na serikali katika Katiba.
Taifa leo imepata michoro ya usanifu ambayo inaonyesha kuwa jengo hilo la kanisa litakuwa na uwezo wa kuhudumia hadi waumini 8,000 na litagharimu walipa ushuru karibu Sh1.2 bilioni.
Jengo hilo, lililopambwa kama ‘Cathedral’, linaundwa na Skair Architects Limited, lina madirisha marefu na picha za setilaiti zinaonyesha ujenzi unaoendelea karibu na eneo la kutua helikopta ya Rais.
Ikulu haikutoa majibu kuhusu mradi huo, licha ya Taifa Leo kutaka kujua nia ya ujenzi huu, kama unaungwa na vigezo vya kikatiba, na kiasi utakachogharimu walipa ushuru.
Awali, Rais Ruto alionyesha wazi nia yake ya kujenga kanisa kuhakikishia imani yake ya Kikristo.
Huku akiwa Naibu Rais, alikuwa na sehemu ya ibada katika makazi rasmi ya Karen, iliyofadhiliwa kwa pesa za umma.
Alitumia hiyo kukaribisha viongozi wa dini akijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2022. Ujenzi wa sehemu hiyo ya ibada ulilaumiwa kwa madai kuwa ulivunja Katiba.
Hata hivyo, alipinga wakosoaji na kutangaza atajenga nyingine kubwa zaidi akiingia madarakani.
“Tulijenga moja katika kasri la hasla, lakini tulikumbana na changamoto. Nitajenga nyingine kubwa ili nchi hii iendelee kutambua uwepo wa Mungu,” alisema Rais Ruto Julai 17, 2022 akihudhuria ibada kanisani Juja.
Ingawa Rais hajathibitisha rasmi ujenzi huu mpya, aliupigia debe mwanzo wa mwaka huu kwenye ibada iliyofanyika Dagoretti Kaskazini.
“Kuna uwanja maalum ninaofanyia kazi, mahsusi kwa watu wanaosali na wanaohubiri,” alisema Rais Januari 11 wakati wa ibada katika Kanisa la United Pentecostal Church of Kenya, Dagoretti Kaskazini.
“Ninataka ninyi (viongozi wa dini) mje mbariki uwanja huo mara utakapokamilika. Nitawaalika ili tuzungumze.”
Taifa Leo iliwasiliana na wasanifu wa jengo ili kupata maoni yao kuhusu hali ya mradi huo.
Mwanzoni, msanifu mkuu alikana kuwa kampuni yake inajenga chochote katika Ikulu ya Nairobi. Baadaye tulimpa picha na michoro ya jengo hilo zinazoonyesha wazi kuwa kampuni yake ndiyo inayohusika, tukimtaka atoe kauli rasmi.
Alijibu kwa kuuliza ni kwa nini tunaamini kuwa jengo hilo lipo katika Ikulu. Baadaye, alitoa matusi na kudai kuwa Taifa Leo inapaswa kuacha “kuiandama” kuhusu mradi huo. Simu, ujumbe na barua pepe zilizofuata hazikujibiwa.
Muundo wa kanisa hilo ni wa kipekee, ukichanganya usanifu wa kale wa kiyunani na ule wa kisasa. Lina nguzo mbili kubwa langoni na madirisha makubwa ya mviringo. Mnara mkuu wa jengo hilo umewekwa msalaba mkubwa juu, ishara ya wazi ya maana ya kidini ya jengo hilo na kwamba linaonekana kutoka mbali. Msalaba mmoja upo mbele na mwingine nyuma, lakini ule wa mbele ndio unaonekana zaidi.
Ndani ya kanisa, kuna mistari minne ya viti vya waumini katika ukumbi mkuu, yenye uwezo wa kuketi hadi waumini 8,000.
Pia kuna milango mingi ya kuingilia, vyumba vya kuhifadhia vitu, vyoo, na njia za kupitishia watu kwa udhibiti bora wa umati. Kila upande wa ukumbi mkuu kuna vyumba viwili vya maombi pamoja na vyumba vingine vya ziada kama vile ofisi na vyoo.
Jengo hilo lina orofa mbili kuu: sakafu ya ukumbi mkuu na roshani mbili za kuketi watu upande wa juu.
Kanisani pia kuna vyumba vinne vya maombi binafsi na chumba kimoja kikubwa cha familia. Mandhari ya nje ya kanisa wakati wa usiku huangazwa kwa taa za LED, huku mlango wa mbele ukiwa wa kioo kikubwa kinachopenya kuona ndani.
Kulingana na Ibara ya 8 ya Katiba, serikali hairuhusiwi kuongoza au kuunga mkono dini yoyote. Taasisi za umma, ikiwemo ofisi ya Rais, hazipaswi kuonekana kupendelea mfumo fulani wa kidini.
Wakili Kibe Mungai, anasema ujenzi wa jengo la kidini ndani ya Ikulu ni kinyume cha Katiba ambayo inataka sekta ya umma kutopendelea dini yoyote.
Anasema Ikulu ni ardhi ya umma, inayolindwa na ni kwa ajili ya kazi za Rais, si sehemu ya ibada.