Habari za Kitaifa

Ufisadi: Kenya yalala darasani

January 31st, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WANDERI KAMAU

HALI ya ufisadi iliongezeka nchini mwaka 2023, imeonyesha ripoti mpya iliyotolewa Jumanne na shirika la Transparency International (TI).

Ripoti kuhusu Hali ya Ufisadi Afrika ilionyesha kuwa Kenya ilishusha alama zake kutoka 32 hadi 31.

Kulingana na mfumo unaozingatiwa kutoa alama kwa nchi husika na shirika hilo, alama zinazokaribia 100 huonyesha nchi ina kiwango cha chini cha ufisadi, huku zile zinazokaribia 50 zikiashiria kiwango cha juu sana cha ufisadi.

Kulingana na utathmini wa miaka kumi uliofanywa na shirika hilo, Kenya ilipata alama bora zaidi mnamo 2022—ilipozoa alama 32—huku ikipata alama za chini zaidi mnamo 2015, ilipozoa alama 25.

“Moja ya sababu ambazo zimechangia Kenya kushusha alama zake mnamo 2023 ikilinganishwa na 2022 ni kucheleweshwa kwa baadhi ya kesi zinazohusiana na ufisadi. Baadhi ya kesi zimekuwa zikicheleweshwa katika hali zisizoeleweka, huku nyingine zikifutiliwa mbali na washukiwa wakuu kuachiliwa huru,” ikasema ripoti hiyo.

Ikaongeza: “Mfano bora ni kufutiliwa mbali kwa kesi ya ufisadi ya ujenzi wa mabwawa tata ya Arror na Kimwarer. Ni kesi ambayo kufutiliwa mbali kwake kumebaki kuwa tata.”

Ripoti ilieleza kuwa kutofaulu kwa kesi kubwa kama hizo kumeshusha imani ya raia kwenye utendakazi wa Afisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kwenye vita dhidi ya ufisadi.

Rwanda ndilo taifa lenye kiwango cha chini zaidi cha ufisadi katika ukanda wa Afrika Mashariki, kwani ilizoa alama 53. Mnamo 2022, ilizoa alama 51.

Tanzania ndiyo iliifuata Rwanda kwa kuzoa alama 40.

Hata hivyo, Kenya iliibuka bora kuliko Uganda na Burundi, zilizoorodheshwa kuwa na kiwango cha juu cha ufisadi zaidi.