Habari za Kitaifa

Uganda yaachilia wanaharakati wa Kenya iliyokana kuzuilia

Na  SHABAN MAKOKHA November 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

 Furaha ilitanda nchini Kenya baada ya wanaharakati wawili, Bob Njagi na Nicholas Oyoo, waliokamatwa nchini Uganda na kuripotiwa kutoweka, kurejea nchini na kuungana na familia zao.

Kamishna wa Kaunti ya Busia, Bw Mwachaunga Chaunga, alithibitisha alipokea wanaharakati hao saa nane usiku wa kuamkia Jumamosi.

“Kuachiliwa kwao kulitokana na mazungumzo makali ya kidiplomasia kati ya serikali ya Kenya na ile ya Uganda,” alisema Bw Chaunga.

Wawili hao walisindikizwa hadi mpaka wa Kenya na Uganda eneo la Busia na Balozi wa Kenya nchini Uganda, Bw Joash Maangi, kisha wakakabidhiwa kwa maafisa wa Kenya waliokuwa wakiwasubiri.

Bw Chaunga alisema kuwa Njagi na Oyoo walipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Busia kwa uchunguzi wa kiafya na ilibainika wako katika hali nzuri.

Kwa upande wake, Bw Maango alisema kuwa kuachiliwa kwao kulifanyika baada ya mazungumzo marefu kati ya ubalozi wa Kenya mjini Kampala na maafisa wa Uganda.

“Kuachiliwa kwa ndugu zetu hawa kunadhihirisha ushirikiano wa karibu wa kikanda kati ya Kenya na Uganda na hata mataifa jirani,” alisema Bw Maangi.

Wanaharakati hao wawili wa haki za binadamu walitoweka nchini Uganda baada ya kuripotiwa kutekwa na wanaume waliokuwa na silaha walipokuwa wakihudhuria kampeni za kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine.

Awali, polisi wa Uganda walikanusha kuwazuilia, hali iliyozua ghadhabu kutoka kwa mashirika mbalimbali yaliyoshinikiza serikali ya Uganda kufichua waliko na kuhakikisha usalama wao.

Chama cha Wanasheria wa Kenya (LSK), Amnesty International Kenya na Vocal Africa waliandika barua ya pamoja kwa Ubalozi wa Uganda nchini Kenya wakieleza kuwa kutekwa kwa wanaharakati hao ni “kisa kingine cha kutisha katika mfululizo wa matukio ya utekaji nyara na watu kutoweka katika ukanda huu.”