• Nairobi
  • Last Updated June 15th, 2024 1:54 PM
Ugavi wa mapato hauwezi kutegemea idadi ya watu, CRA yaambia Gachagua

Ugavi wa mapato hauwezi kutegemea idadi ya watu, CRA yaambia Gachagua

NA BARNABAS BII

TUME ya Ugavi wa Mapato (CRA), imeingilia mjadala wa mfumo wa kutenga pesa kwa kaunti kwa kutegemea idadi ya watu, badala ya ukubwa wa eneo, unaoungwa mkono na Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, ikisema hauwezekani.

CRA ilisema kwamba kampeni inayoendelea ya kura moja -mtu mmoja -shilingi moja, ambayo inavumishwa na Bw Gachagua, itarudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana katika usambazaji wa rasilimali kwa Wakenya wote kwa usawa.

Tume hiyo inashikilia kuwa hakuna kaunti iliyopendekeza kile kinachoitwa mtu-mmoja-kura-moja- shilingi moja kama kigezo cha kugawa mapato, ikisema kuwa utaratibu wa sasa ulinuiwa kuwezesha maendeleo kwa Wakenya wote kwa usawa.

“Kwa mtazamo wa kitaalamu, mtu mmoja -kura moja- shilingi-moja ni kigezo kimoja tu miongoni mwa vingine vinavyotumiwa.
“CRA inasema haiwezi kutumia kipengele kimoja kutenga rasilimali.

“Kama tume, hatutazingatia hilo kwa sababu halijatoka kwa kaunti yoyote,” alisema kamishna wa CRA Hadija Juma, katika warsha ya maafisa wa kaunti ya Uasin Gishu kuhusu jinsi ya kuimarisha vyanzo vyao vya mapato.

Alisema CRA itaendelea kuhakikisha kuwa kuna maendeleo sawa nchini, akieleza kuwa pendekezo hilo litanufaisha tu baadhi ya Wakenya.

“Tunataka kila Mkenya humu nchini ajihisi kuwa ni Mkenya. Tunataka maendeleo yafike kila kona ya nchi hii na tunapotumia kigezo cha mtu mmoja-kura moja-shilingi moja, Wakenya wengine wataachwa nyuma na kama CRA hatutaki Mkenya yeyote aachwe,” aliongeza Kamishna Juma.

Gavana wa Uasin Gishu, Jonathan Bii alipuuzilia mbali pendekezo hilo akisema halitekelezeki na kuongeza kuwa rasilimali za kitaifa zinafaa kufikia Wakenya wote.

“Je, mfumo huu wa ugavi wa mapato utawezaje kushughulikia maslahi ya mkulima mkubwa ambaye analima mashamba makubwa ili kuwapa Wakenya wengine chakula?” alishangaa Gavana Bii.

Gavana huyo alitoa wito wa kuwepo kwa mfumo wa ugavi wa mapato ambao utakidhi maslahi ya Wakenya wote, akisema kuwa wakulima katika eneo la North Rift pia wanachangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Gavana Bii aliunga mkono viongozi kutoka kaunti kame na zenye kiangazi ambao wametaja mfumo huo unaoshinikizwa na baadhi ya viongozi kutoka eneo la Kati kama kuendeleza udhalilishaji wa baadhi ya jamii bila sababu.

Viongozi hao wameapa kutetea ugavi wa mapato ya mtu mmoja kwa kura moja na kilomita moja, ambao huenda ukapandisha zaidi joto la kisiasa nchini.

Wakati huo huo serikali nyingi za kaunti katika eneo la North Rift zinaweza kupoteza mamilioni ya pesa za miradi ya maendeleo iliyokwama, marupurupu ya usafiri na malazi ya maafisa wakuu ambayo hayawezi kuthibitishwa, na za kulipa madeni makubwa licha ya kupokea ufadhili mkubwa kutoka kwa Hazina ya Kitaifa.

Baadhi ya kaunti zimelazimika kuchukua hatua za kufanya marekebisho baada ya kutajwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kama zinazotekeleza ubadhirifu wa fedha za umma kwa kushindwa kulipa madeni.

  • Tags

You can share this post!

Mkenya Cheruiyot Kirui alielewa kibarua cha kuukwea Mlima...

Cheo cha nuksi: Mikosi ilivyoandama manaibu rais Kenya...

T L