Habari za Kitaifa

Uhaba wa vitabu washuhudiwa shule zikifunguliwa

Na Na WAANDISHI WETU January 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

UHABA  wa vitabu vya shule za msingi unashuhudiwa nchini, baadhi ya wamiliki wa maduka ya vitabu wakisema walipokea asilimia 60 pekee ya mahitaji yao.

Mkurugenzi wa duka la vitabu la Kimji Devshi, mojawapo ya wasambazaji Kaunti ya Nyeri, Bw Khilan Shah, alisema uhaba huo unawaathiri zaidi wanafunzi wa PP1 hadi Gredi ya 4.

Alieleza kwamba uhaba huo unachangiwa na wachapishaji waliokabidhiwa kandarasi na serikali ambao wamechelewesha uchapishaji.

“Vitabu havipatikani. Mzazi anaagiza vitabu 10 kwa darasa moja lakini tunapata vinne pekee. Bei ya vitabu vilivyoko iko juu, na hali hii inawaumiza wazazi ambao tayari wanakabiliana na gharama kubwa ya maisha,” alisema.

Katika maneo mengi wauzaji vitabu walisema vitabu vya Gredi ya Tisa vipo lakini wanakumbwa na changamoto kupata vitabu vya Gredi ya kwanza hadi sita.

Katika kaunti ya Murang’a, Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Elimu, Bw Joe Nyutu, alisema wazazi wanapaswa kupewa muda wa kununua vitabu vya Gredi ya Tisa.

“Ni kweli kuwa kufikia Jumapili, vitabu havikuwa vinapatikana kwenye soko. Serikali ilikosa sera na imeshangaza wadau wote kutokana na uhaba huo,” alisema Bw Nyutu.

Mzazi kutoka Murang’a, Bi Elizabeth Soliyo alisema baadhi ya vitabu vinapatikana kwa bei ghali.

Mfanyabiashara, Bw Martin Thuo, alisema kuna mkanganyiko kuhusu orodha ya vitabu vilivyoidhinishwa.

IMETAFSIRIWA NA FRIDAH OKACHI