Uhuru ajiandaa kumpa Matiang’i uongozi Jubilee
RAIS Mstaafu Uhuru Kenyatta anapima uwezekano wa kumpa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i uongozi wa Jubilee kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2027.
Taifa Leo imebaini kuwa mpango huo unaendelea kusukwa tayari kutekelezwa katika Kongamano Kuu la Kitaifa la Wajumbe (NDC) mnamo Septemba 26, 2025.
Ni katika kongamano hilo ambapo wanachama watajadili na kuafikiana iwapo Dkt Matiang’i atapewa uongozi wa Jubilee na kutajwa mwaniaji wake wa urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Aidha imebainika kuwa wakati wa kongamano hilo, Jubilee pia itawazia kujiondoa kwenye Muungano wa Azimio la Umoja.
Hii ni baada ya kiongozi wa Azimio Raila Odinga ambaye aliungwa mkono 2022 na vyama tanzu vya Azimio ikiwemo Jubilee kuamua kufanya kazi na serikali.
Narc Kenya ambayo sasa inafahamika kama PLP pamoja na DAP-Kenya ni vyama tanzu ambavyo tayari vimeasisi mchakato wa kujiondoa Azimio.
Katika kujijenga upya na kujiandaa kwa 2027, Jubilee inapanga kuingia kwenye muungano na DAP-K, UPA, Chama cha Kazi chake Moses Kuria, Kanu ya Gideon Moi na PNU ya aliyekuwa Gavana wa Meru Peter Munya.
Dkt Matiang’i amekuwa akipigiwa upato achukue usukani wa UPA, chama kinachoongozwa na Gavana wa Nyamira, Amos Nyaribo, chenye ufuasi sana eneo la Gusii.
Seneta wa Kisii, Richard Onyonka jana alisema kuwa kuna mazungumzo yanayoendelea kumfanya Dkt Matiang’i kiongozi wa Jubilee na mwaniaji wake wa urais 2027.
“Ni suala ambalo liko mezani na tunalitathmini kwa kuzingatia nafasi nyingine pia kabla ya kufanya uamuzi,” akasema Bw Onyonka mwandani wa Matiang’i.
Seneta huyo alikiri kuwa kuna mgawanyiko mkubwa; baadhi wakitaka Dkt Matiang’i ajiunge na Jubilee ambayo tayari inaonekana kama cha kitaifa.
Kwa upande mwingine wengine wanataka awe kiongozi wa UPA ili awe na chama ambacho kina uungwaji mkono kwenye ngome yake ya kisiasa.
“Tunaangalia pande zote lakini mwaamuzi ni Dkt Matiangí mwenyewe. Akikubali kuwa kiongozi wa Jubilee tutamuunga mkono,” akaongeza.
Ingawa hivyo, wasiomtaka Dkt Matiangí aingie Jubilee wanasema akijiunga na chama hicho uaminifu wake lazima utakuwa kwa Bw Kenyatta.
Katibu Mkuu wa Jubilee Jereamiah Kioni amewahi kunukuliwa akisema chama hicho kitamuunga mkono Dkt Matiangí mnamo 2027.
Hata hivyo, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amekuwa akipinga Dkt Matiang’í kujiunga na Jubilee akimtaka ajiunge na UPA ili kujihakikishia uungwaji mkono wa nyumbani, ushawishi na usemi wa kisiasa.
“Ili aheshimiwe pamoja na jamii ya Gusii lazima awe na chama cha nyumbani kabla ya kuenda vita nje,” akasema Bw Gachagua katika mahojiano na kituo cha redio cha Egesa.