Ujangili wachacha Meru Gavana Isaac Mutuma akilaumu Murkomen kwa kulaza damu
LICHA ya ahadi ya kuhakikishiwa usalama, ujangili bado unaendelea kuwaandama wakazi wa eneo la Buuri, Kaunti ya Meru.
Mnamo Novemba 28, 2025 genge la watu 40 waliobeba silaha lilivamia kijiji cha Maili Saba.
Wakionekana wakiwa na mikakati, baadhi walisimama nje kukagua hali, wengine wakivamia maboma kuchukua mifugo na pia kuna wale ambao walifyatua risasi hewani kuwahofisha wenyeji.
“Walikuwa wamebeba bastola na bunduki kubwa. Wakati ambapo walikuwa wakiondoka, nilikuwa nimeibiwa ngómbe 29, mbuzi 22 na kondoo wanane,” akasema Askofu Richard Mwenda.
Uvamizi huo wa majangili ulichangia uvamizi mwingine ambao uliendeshwa na majangili Maili Saba na vijiji vya karibu.
Kutokana na kuongezeka kwa visa hivyo vya uvamizi, wengi kutoka Lokesheni ya Kithima sasa wanauza mifugo yao ili kuepuka hasara zaidi.
Wanakijiji pia wanawashutumu wenzao kwa kushirikiana na wezi hao, katika kile wanachosema ni wizi ambao umepangwa vizuri sana maarufu kama ‘Meru ATM’.
“Ndani ya miezi mitatu, nyumba nane zimevamiwa na kwetu kumeathirika zaidi huku zaidi ya mifugo 300 ikiibwa. Familia sasa zimerejea kwenye umaskini hasa kipindi hiki cha sherehe na ikumbukwe kuwa kutakuwa na suala la karo Januari ikifika,” akasema Askofu Mwenda.
Ingawa kulikuwepo visa vya ujangili mapema mwaka huu, vimeongezeka sana kuanzia baadaye Septemba. Visa hivyo vimesababisha maandamano si mara moja kwenye barabara ya Nanyuki-Isiolo.
Katika tukio la hivi punde mnamo Desemba 8, Stephen Guantai kutoka Maili Nane alinusurika kifo pembamba baada ya risasi kumkosa padogo kichwani.
Majangili watano wakiwa wamejihami kwa bunduki walivamia nyumbani kwake na kuwaiba ngómbe wanane.
“Walipiga risasi mlangoni kututishia kisha wakachukua fahali watatu na ngómbe wa maziwa. Wanaenda kutoka nyumba moja hadi nyingine kuiba mifugo wetu,” akasema.
Diwani wa zamani Patrick Gakuubi naye alipoteza mbuzi 28 na ng’ombe wanne mapema mwaka huu. Anasema bado usalama ni mbaya na anaiomba serikali iingilie kati kuwasaidia kulinda mali yao.
“Sasa wanalenga maduka pia. Niliibiwa mifugo na vifaa vyangu vya elektroniki kwenye duka langu Maili tano. Tumeitisha usalama lakini hakuna kinachobadilika,” akasema.
Kamishina wa Kaunti ya Meru Jacob Ouma naye alisema usalama umezidishwa na kwamba polisi hawataruhusi wizi zaidi wa mifugo.
Ripoti ya Polisi inaonyesha washukiwa watatu walinyakwa Desemba 12, 2025 kuhusiana na wizi wa mbuzi 26 mkesha wa Sikukuu ya Jamhuri.
Licha ya hakikisho kutoka kwa Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki kuwa operesheni ya kiusalama itaendeshwa, watu wanaendelea kupoteza mali na mifugo yao.
Profesa Kindiki alikuwa amesema operesheni hiyo itaendeshwa kaunti za Samburu, Meru na Isiolo.
Gavana wa Meru Isaac Mutuma naye ameshutumu Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen kwa kukosa kutimiza ahadi ya kuamrisha operesheni ya kiusalama kufikia Desemba 5.
Alikuwa amekutana na wakuu wa polisi kutoka eneo hilo mnamo Desemba 2 kutokana na hali ya usalama eneo hilo. Hii ni baada ya watu watatu akiwemo maafisa wawili wa polisi wa akiba kuuawa mwezi uliopita.
Wiki mbili zilizopita, Profesa Kindiki aliwaonya majangili hao lakini siku chache zilizofuata bado wakawavamia wakazi.