Ujangili: Wahubiri walilia Ruto
ERIC MATARA Na GEOFFREY ONDIEKI
VIONGOZI wa kidini kutoka kaunti sita eneo la Bonde la Ufa wameelezea wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa ukosefu wa usalama Kaskazini mwa Bonde la Ufa na kumrai Rais William Ruto kuingilia kati binafsi ili kukomesha kero hilo.
Viongozi hao kutoka kaunti za Baringo, Nakuru, Bomet, Kericho, Samburu na Narok wakiongozwa na Baraza la Kitaifa la Makanisa Nchini (NCCK) Kusini mwa Bonde la Ufa, Ernest Ng’eno, vilevile wanataka serikali kuchukua hatua kali dhidi ya wanasiasa na watu binafsi wanaohusika na kuchochea shughuli za ujangili eneo hilo.
Watu zaidi ya 10 wamepigwa risasi na kuuawa katika maeneo ya Baringo,Samburu,Laikipia na Elgeyo Marakwet katika muda wa mwezi mmoja uliopita.
“Tunatoa wito kwa Rais William Ruto kuingilia kati na kuchukua hatua kali zaidi ili kudhibiti hali ya ukosefu wa usalama. Watu zaidi wanaendelea kuuawa katika sehemu za Baringo na Samburu na majangili, hali hiyo inahofisha,” alisema Bw Ng’eno.
‘Serikali pia inapaswa kuhusisha viongozi wa kanisa katika kuzungumza na jamii na mikakati ya kuleta amani ikiwemo kuimarisha imani ya umma kwa polisi ili kuwezesha usambazaji wa habari za ujasusi mapema miongoni mwa jamii,” alisema.
Viongozi hao wa kidini waliozungumza katika Kanisa la Kianglikana la St’ Luke, mjini Narok pia walitoa wito kwa serikali za kaunti katika maeneo yanayoathiriwa na ujangili kufanya hima kutoka huduma bora na kupatia kipaumbele mahitaji muhimu ya jamii ili kustawisha maendeleo.
Wito wao umejiri wakati ambapo mashambulizi yamezidi Kaunti za Baringo na Samburu katika muda wa wiki moja iliyopita na kusababisha vifo na wengine kulemazwa.
Kisa cha kutisha majuzi, kilitendeka saa chache tu baada ya mazishi ya Diwani wa Wadi ya Angata Nanyekie Paul Leshimpiro, aliyeuawa kinyama na majangili wiki iliyopita.
Katika shambulio hilo lililotendeka Jumamosi usiku, mhasiriwa ambaye ni mchungaji alipigwa risasi na kuuawa katika eneo la Lolmolog katika tukio lililotikisa kijiji hicho kilichokuwa bado kinaomboleza vifo vya wakazi wawili, Baba na mwanawe waliouawa wiki jana.
Kulingana na Kamanda wa Polisi Kaunti ya Samburu, Thomas Ototo, majangili waliojihami walivamia kijiji cha Lolmolog Jumamosi jioni wakilenga kuiba mifugo.
Bw Ototo alieleza Taifa Leo kuwa mhasiriwa aliaga dunia papo hapo baada ya tukio hilo.
‘Majangili walivamia kijiji saa za jioni na walikuwa wanalenga kuiba mifugo. Walifukuzwa na polisi wetu wa akiba lakini tukapoteza mchungaji wa mifugo katika harakati,” Bw Ototo.