Habari za Kitaifa

Ujanja wanaotumia wabunge kutuliza ghadhabu za raia


WABUNGE ambao waliunga mkono Mswada wa Fedha 2024 kutoka eneo la Magharibi sasa wameanza kutumia ujanja kuhepa ghadhabu za raia katika maeneobunge yao.

Emmanuel Wangwe (Navakholo) na Malulu Injendi wa Malava ni kati ya wabunge ambao wikendi walishiriki hafla ya miradi ya maendeleo katika maeneo yao wakilenga kusahaulisha raia kuhusu uamuzi wao wa kuunga mswada huo.

Wawili hao Jumatatu, Julai 8, 2024 walisambaza tarakilishi katika shule mbalimbali kwenye maeneobunge yao na hotuba zao zikiminikia kile ambacho watawafanyia raia.

Mbunge wa Matungu Peter Nabulindo naye alinyenyekea sana alipohudhuria mazishi  na ibada katika eneobunge lake kiasi kuwa baadhi ya wapigakura walionekana wakimhurumia.

Christopher Aseka wa Khwisero pia hakuwa na makeke kama kawaida yake alipohudhuria hafla ya elimu katika Shule ya Upili ya Emalindi.

Hata hivyo, mbunge wa Ikolomani Bernard Shinali alizomewa katika hafla moja ya mazishi iliyohudhuriwa na Gavana wa Kakamega, Fernandes Barasa na Seneta Bonny Khalwale.

Wanasiasa hao walihudhuria mazishi ya Mkurugenzi wa Sekta ya Kilimo George Mbakaya.

Baadhi ya wakazi wa Matungu walimhurumia Bw Nabulindo alipohudhuria ibada katika kanisa la Revival kijiji cha Lairi ambako ni nyumbani kwake.

Vijana, akina mama na wazee walimwombea na kusema kuwa wamemsamehe kutokana na hatua aliyochukua ya kuunga mkono mswada huo.

“Tumefurahi kuona amerejea, hatuna shida naye ila sasa anaelewa kuwa wananchi ndio wenye sauti katika masuala ya taifa,” akasema mkazi Gaudenzia Odhiambo.

Aliposimama kuhutubu mbunge huyo alinyenyekea na kusema kuwa uamuzi wake ulitokana na imani kuwa waliomchagua, wangenufaika kimaendeleo.

“Mmeonyesha ukomavu kwa kutoandamana baada yangu kupigia kura Mswada wa Fedha 2024. Mmeonyesha kuwa mlimchagua mtu ambaye mnamwaamini wala si kwa sababu ya chama,” akasema Bw Nabulindo.

Licha ya kuchaguliwa kupitia ODM Bw Nabulindo, Aseka na Wangwe walienda kinyume na agizo la chama hicho la kupinga mswada huo.

Kutokana na maandamano ya Gen Z, Rais William Ruto alilazimika kuondoa mswada huo kabisa.