Ukabila wachacha katika kaunti kuajiri wafanyakazi – Ripoti
NA ERIC MATARA
KAUNTI 30 zimemulikwa kwa kukosa kutimiza usawa wa kikabila katika kuajiri wafanyakazi wake, kulingana na ripoti mpya iliyotolewa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwenye bajeti ya 2022/2023.
Ripoti hiyo inafichua kwamba kaunti hizi hazijazingatia viwango vya kikatiba vya kuwa na asilimia 30 ya wafanyakazi wake kutoka makabila mengine kando na wenyeji.
Kaunti 10 zimetambulishwa ambapo asilimia 90 ya wafanyakazi wake wanatoka kabila moja na kuacha asilimia 10 pekee kuwakilisha makabila mengine.
Mkaguzi Mkuu wa serikali Nancy Gathungu alifichua kuwa ni kaunti 17 pekee zimeweza kuzingatia hitaji hili kwa kuwa na chini ya asilimia 40 ya wafanyakazi kutoka kabila moja.
Licha ya sheria inayoagiza kuhakikisha ujumuishaji katika ajira, baadhi ya kaunti zimeajiri wafanyakazi wapya kutoka jamii wenyeji, hivyo kuzidisha tofauti iliyopo.
“Udadisi wa rekodi za data kuhusu Malipo ya Wafanyakazi (IPPD) za mwezi wa Juni, 2023, ulidhihirisha kuwa karibu kaunti 10 zilikuwa na asilimia zaidi ya 90 ya wafanyakazi kutoka kabila la wenyeji. Hii ni kinyume na Kipengee 7 (2) cha Sheria kuhusu Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, 2008, inayosema hakuna asasi ya umma itakayokuwa na zaidi ya thuluthi moja ya wafanyakazi wake kutoka kabila moja,” inasema ripoti.
Katika Kaunti ya Bomet, ilibainika kuwa miongoni mwa wafanyakazi 3,566, 3467 (asilimia 97) wanatoka kabila la Wakalenjin.
Wafanyakazi 3,571, miongoni mwa 3,738 katika Kaunti ya Nandi (asilimia 96) ni Wakalenjin.
Katika Kaunti ya Nyandarua, wafanyakazi 2, 264 miongoni mwa 2,373 (asilimia 95) wanatoka kabila la wenyeji, Agikuyu.
Wafanyakazi 1,474 miongoni mwa jumla ya wafanyakazi 1,559 wa kudumu Elgeyo Marakwet wanatoka kabila la Wakalenjin (asilimia 95).
Isitoshe, katika mwaka huo, kaunti iliajiri maafisa wapya 36 wote kutoka kabila la wenyeji kinyume na sheria.
Huko Nyamira, wafanyakazi 3,734 miongoni mwa 3,955 wanatoka kabila la wenyeji, Abagusii.
Nyeri, Murang’a na Kirinyaga kila moja ilikuwa na asilimia 92 ya wafanyakazi wake kutoka jamii ya Agikuyu.
Katika kaunti ya Kakamega, wafanyakazi 6, 251 miongoni mwa 6, 876 wanatoka kabila la Waluhya huku 4,205 miongoni mwa wafanyakazi 4,695 katika Kaunti ya Kitui wakiwa Wakamba.
Katika kaunti ya Siaya, miongoni mwa wafanyakazi 1,950, 1,697 wanatoka kabila la wenyeji, Waluo.
Miongoni mwa wafanyakazi 6,621 Kaunti ya Kiambu, 5,667 ni wenyeji.
Huko Uasin Gishu, wafanyakazi 4,030 wa kudumu miongoni mwa 4,707 ni Wakalenjin.
Wafanyakazi 2,032 miongoni mwa 2,446 ni wenyeji kutoka kabila la Wamaasai katika Kaunti ya Samburu.
Miongoni mwa wafanyakazi 4,508 wa Kilifi, 3,564 ni wenyeji.
Asilimia 77.7 ya wafanyakazi wa Garissa wanatoka kabila la wenyeji.