Habari za Kitaifa

Ukijiamini, njoo tena kwa kura za udiwani Mbeere, wandani wa Ruto wamcheka Gachagua

January 20th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

MAWAZIRI wawili na baadhi ya wabunge kutoka Kaunti ya Meru wamesema kuwa watahakikisha upinzani unashindwa tena katika chaguzi ndogo za udiwani zinazokuja katika eneobunge la Mbeere Kaskazini.

Mawaziri Geoffrey Ruku (Utumishi wa Umma), Eric Muga (Maji) na wabunge Paul Mwirigi (Igembe Kusini), Dan Kiili (Igembe ya Kati) na Mpuru Aburi (Tigania Mashariki) wamemshutumu aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Waziri wa zamani wa Kilimo Mithika Linturi kwa kupanda mbegu za kugawanya Mlima Kenya.

Walisema wanataka DCP iwasilishe wagombeaji katika maeneo ya udiwani ya Evovure na Muminji ili wapambane nao debeni.

Viongozi hao wakizungumza eneobunge la Igembe Kusini mnamo Jumapili, waliwashutumu Mabw Gachagua na Linturi kwa kuendesha kampeni ya kupaka serikali kuu tope baada ya kufeli kwenye majukumu ambayo walipewa na Rais William Ruto.

Upinzani umesema vyama vya DP na DCP vitawasilisha wagombeaji kwenye wadi za Muminji na Evuvore.

Bw Ruku alipuuza madai kuwa DCP ni maarufu Mlima Kenya akisema uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini mnamo Novemba mwaka jana ulionyesha jinsi chama hicho kinaendelea kuisha.

“Tumetoa notisi kwa upinzani Mlima Kenya na kwa sababu tuna chaguzi mbili ndogo, nawataka wawasilishe wagombeaji wao kama wanaamini chama chao ni imara. Tutawashinda kwa kura nyingi,” akasema Bw Ruku.

Alisema Rais Ruto ana uungwaji mkono mkubwa eneo hilo kwa sababu upinzani umekosa ajenda ya maendeleo kwa nchi.

Bw Muga alitetea serikali, akisema miradi mingi ya unyunyuziaji mashamba maji na miradi ya maji inaendelea kutekelezwa nchini.

“Rais Ruto ana mpango mahususi wa kuhakikisha Kenya ina maji ya kutosha. Mpango wetu ni kuhakikisha kwamba wakulima si lazima wasubiri mvua ili washiriki upanzi,” akaongeza.

Wabunge hao watatu walimshambulia Bw Linturi kutokana na kauli yake kuwa wabunge kutoka Meru wamegeuka vibaraka wa Rais Ruto.

Bw Linturi amekuwa akiwashambulia wabunge hao kwa kukosa kutekeleza majukumu yao ya kuwajibisha serikali ili iimarishe utendakazi wake.

“Kama viongozi waliochaguliwa, tunaongea kwa niaba ya watu kutoka eneo hili. Watu waliopewa kazi na serikali lakini wakakosa kuwajibika na kulemewa na kazi hawawezi kuzungumza kwa niaba yetu,” akasema Bw Mwirigi.

Bw Ruku alidai kuwa Bw Linturi alikuwa na utendakazi duni wakati ambapo alikuwa waziri wa Kilimo na hana kazi yoyote ya kukosoa serikali.

“Alikosa kufanya kazi alipopewa nafasi, wakulima waliteseka kutokana na mbolea feki. Kama mwanakandarasi, hakumaliza barabara ambazo zilianzishwa na serikali iliyopita,” akasema Bw Ruku.

Naye Bw Mugaa alimshutumu Bw Linturi kwa kuwakosea heshima viongozi wa Meru kwa kueneza siasa za uchochozi.

“Linturi akome kuwakosea heshima viongozi wachanga. Anastahili kuniheshimu kwa sababu alinituza kama mwanafunzi bora Igembe Kusini mnamo 2003 alipokuwa mbunge,” akasema.

Viongozi hao walitetea utawala wa Rais Ruto kuhusiana na madai kuwa unabagua Mlima Kenya, akisema mawaziri wengi wanatoka eneo hilo.