Habari za KitaifaMakala

Ukitaka kutoza Wakenya ada ya barabara, jengeni zenu, Kalonzo afokea Ruto

Na LABAAN SHABAAN August 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BAADHI ya vyama tanzu vya Muungano wa Azimio vinajipanga kutwaa jukumu rasmi la upinzani baada ya baadhi ya wanachama wa ODM kukabidhiwa majukumu katika serikali ya Kenya Kwanza.

Viongozi wa vyama vya Wiper Democratic Party, Jubilee na Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) wamesema wanachukua hatua hii kuepusha taifa na uongozi wa udikteta.

Waliongozwa na vinara wa Azimio wakiwemo Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni na Kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa.

Vinara hawa walifichua kuwa wote wamekuwa na mikutano ya baraza la kitaifa na kuamua kusimama na Wakenya wanaopinga sera dhalimu za matozo ya juu ya ushuru.

“Hatuwezi kujiunga na serikali kwa sababu tumeamua kusimama na Wakenya. Tumewaruhusu waingie serikalini na tutabaki na kiongozi wetu Kalonzo Musyoka,” alitangaza Bw Wamalwa.

Pamoja nao katika kikao katika Kaunti ya Embu Jumapili, viongozi hao waliungana na aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu.

Bw Waititu alisema kuwa aliwakilisha sehemu ya viongozi wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) wasioridhishwa na sera za serikali.

Bw Waititu alisema wao wanajiunga na upinzani ili kushinikiza uwajibikaji serikalini.

Bw Kalonzo ambaye ametajwa kuwa ‘kiongozi’ wa muungano huo, amesema wameamua kuwa katika upande wa vijana ambao walifaulu kuzima Mswada wa Fedha wa 2024.

Amesema atapinga jaribio lolote la kuongeza ushuru uliopendekezwa katika mswada wa fedha ulioibua utata.

“Tumeona serikali ikiingiza kodi mpya kama ile ya Ushuru wa Ukarabati wa Barabara na nyongeza ya ada ya umeme. Haya ni matukio ambayo hatutayaruhusu,” aliwaka.

Kadhalika, Bw Kalonzo alisema kuwa muungano huo umepinga kuanzishwa kwa ada ya usafiri katika barabara kuu kama inavyopendekezwa na serikali.

“Kama unataka kuanzisha ada ya barabara, jengeni barabara zenu na usitoze ushuru zile zilizojengwa na Rais Mwai Kibaki. Mkifanya hivi mnavamia mifuko ya Wakenya na tutapinga mpango huo,” Bw Kalonzo aliambia Rais Ruto.

Viongozi hao walishinikiza Wakenya wawe waangalifu wakidai serikali inaelekea katika mfumo wa uongozi wa kiimla.

Wote kwa moto mmoja waliradidi kauli zao za awali kuwa Rais William Ruto ameteka bunge na itakuwa rahisi kwao kupitisha sheria ambazo ni dhalimu kwa wananchi.

Raila hayuko nasi

Akimtakia kheri Kiongozi wa ODM Raila Odinga anapolenga kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Bw Jeremiah Kioni alisema wamejipanga kuwa na kiongozi mpya.

“Sisi ndio upinzani na sisi ni serikali ambayo inatarajiwa (2027). Kiongozi wa Azimio (Kalonzo Musyoka) yuko nasi hapa. Tumekuwa naye kila mahali na tutaendelea,” alisema.

Alirejelea kauli ya Raila Odinga kuwa alishauriwa na Mwenyekiti wa Azimio Uhuru Kenyatta ‘kumsaidia Ruto’ hadi baadhi ya viongozi wa ODM wakajumuishwa katika baraza la mawaziri.

“Uhuru alituonya dhidi ya serikali ya UDA. Hajatuelekeza kuungana na serikali ambayo imeundwa kinyume cha Katiba. Yeye (Uhuru Kenyatta) anasikitishwa kwa nini Wakenya wametelekezwa na serikali,” alisema.

Uongozi bungeni

Bw Kalonzo alitangaza kuwa baraza la usimamizi wa Azimio litakutana Jumatatu kuamua kiongozi mpya rasmi wa upinzani katika Bunge la Kitaifa.

Hii ni baada ya kiongozi wa wachache bungeni Opiyo Wandayi kuteuliwa na kuidhinishwa kuwa Waziri wa Kawi katika serikali.

Kiongozi wa Wiper alieleza kuwa walioteuliwa serikalini hawawezi kuwa katika mrengo wa upinzani.