Habari za Kitaifa

Ukosefu wa maadili ndio unaleta ufisadi, tutatenga fedha zaidi kukuza maadili – Kindiki

Na TITUS OMINDE December 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KAMA njia moja ya kutumia maadili mema katika vita dhidi ya ufisadi, serikali itatenga fedha zaidi mwaka ujao wa kifedha kwa taasisi zilizopewa majukumu ya kudumisha maadili mema katika jamii.

Naibu Rais Kithure Kindiki amesema ukosefu wa maadili na kuenea kwa ufisadi miongoni mwa Wakenya ni kikwazo kwa ndoto ya Rais William Ruto ya kuifanya Kenya kuwa miongoni mwa nchi zilizoendelea duniani kote.

Akihutubu jijini Eldoret Jumatatu, Desemba 8, 2025 wakati wa kufunga rasmi tamasha la Kitaifa la Muziki na utamaduni katika Shule ya upili ya Moi Girls, Profesa Kindiki alisema tishio la ufisadi linaweza kukabiliwa vilivyo kupitia muziki na maadili chanya kupitia kwa utamduni wa Wakenya.

Profesa Kindiki alisema serikali itawekeza katika taasisi zaidi ambazo zina jukumu muhimu katika kukuza maadili miongoni mwa Wakenya.

“Utamaduni na Lugha ina jukumu muhimu kama programu ambayo ni nguzo ya pili ya Ajenda ya mabadiliko kusaidia katika kuimarisha uchumi wa nchi yetu,” akasema Profesa Kindiki.

Alisema ukosefu wa maadili miongoni mwa Wakenya hasa vijana na wataalamu hudidimiza mafanikio ya kiuchumi katika ngazi zote za serikali.

Naibu Rais alikariri haja ya nchi kuwekeza katika wataalamu wa maadili ambao watajitenga na ufisadi katika nyanja zote za maisha kwa kila njia.

Wakati huo huo alipongeza hatua ya Rais William Ruto kuendeleza nchi kupitia ubinafsishaji wa mashirika ya umma akisema kuwa hatua hiyo itawapunguzia Wakenya walipa ushuru mzigo kuchangia katika maendelea ya taifa kupitia kwa ushuru.