Habari za Kitaifa

Ukuruba wa Ruto na Raila waweka hofu wandani katika kambi zao

Na JUSTUS OCHIENG' September 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NDOA ya kisiasa kati ya Rais William Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga sasa imeanza kuzua wasiwasi katika kambi zao huku ikitarajiwa kuibua mpango mpya wa kisiasa nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Ukuruba huo ‘uliohalalishwa’ kupitia mkataba wa ushirikiano ulitiwa saini na wawili hao mnamo Machi 7, ambapo waliazimia kushirikiana chini ya serikali jumuishi.

Katika mrengo wa Kenya Kwanza, wake Dkt Ruto, baadhi ya wandani wake wanasawiri ujio wa Bw Odinga kama tishio kwa ushawishi wao ndani ya serikali.

Katika upande wa ODM, hatua ya Bw Odinga kushirikiana na Rais Ruto inaonekana kama usaliti wa vita vyao dhidi ya Kenya Kwanza.

Wandani wakuu wanahisi kuwa ushawishi wao utayeyuka kwa sababu Bw Odinga sasa anaonekana kujishughulisha zaidi na masuala ya Ikulu.

Aidha, wengine wanahofia kwamba ushirikiano huo utadhoofisha ushawishi wa ODM katika ngazi za mashinani, haswa katika maeneo ambako raia wengi hawaungi mkono serikali.

Nje ya mirengo yao, ushirikiano kati ya Rais Ruto na Bw Odinga umedhoofisha upinzani dhidi ya serikali bungeni na kubadilisha miundo ya miungano.

Huku wawili hao wakivuta upande mmoja kisiasa, vyama vidogo na wanasiasa wanaosaka makuu, wameachwa wakijipanga upya kwani hawaelewi mustakabali wa ushirikiano huo (wa Ruto na Raila).

Juzi wawili hao waliongoza mkutano wa pamoja wa wabunge wa Kenya Kwanza na ODM, kuashiria uwezekano wa ushirikiano wao kudumu hadi katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Sasa wachanganuzi wanasema huenda baadhi ya wandani wa Dkt Ruto na Bw Odinga wakapoteza kwa manufaa ya wawili hao kuelekea uchaguzi huo.

Lakini hata kabla ya kutiwa saini kwa mkataba wa ushirikiano wao, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alikuwa mwathiriwa wa kwanza wa ukuruba huo kwa kutimuliwa kwake.

Baada ya Bw Gachagua kutimuliwa, Oktoba 18, 2024, Rais Ruto alimteua aliyekuwa Waziri wa Usalama Kithure Kindiki kuwa Naibu Rais.

Profesa Kindiki aliapishwa mnamo Novemba 1, mwaka huo kwenye sherehe iliyofana katika uwanja wa KICC, Nairobi.

Lakini huku dalili za Rais Ruto na Bw Odinga kuunda muungano rasmi zikijitokeza, huenda nafasi ya Profesa Kindiki ikatwaliwa katika kile ambacho kimetajwa kama nipe nikupe za siasa za 2027.

Tayari Mbunge wa Nyando, Bw Jared Okello amedai kwamba kwa kuwa ODM sasa ni mshirika mkuu wa UDA, chama hicho cha Chungwa kitadai nafasi ya Naibu Rais.

“Kama chama kikubwa cha kisiasa, kando na urais wadhifa mkuu ambao tutaitisha ni ule wa naibu rais. Aidha, tutaitisha nusu ya idadi ya mawaziri, makatibu wa wizara, mabalozi na wakuu wa mashirika ya serikali,” Bw Okello akaambia Taifa Leo.

Hata hivyo, Bw Odinga amekana madai kwamba chama cha ODM kinamezea mate kiti cha Naibu Rais huku akisifu mtindo wa uongozi wa Prof Kindiki.

Bw Odinga alimtaja Prof Kindiki kama “mpevu kiakili, mwepesi kushirikiana na viongozi wengine na asiyezongwa na hisia za kikabila.”

Aidha, Bw Odinga amepuuzilia mbali madai kuwa anamshurutisha Rais Ruto kumleta kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka upande wao na amtunuku nafasi ya mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu wa 2027.

“Haya sio madai ya ukweli,” akasema.

Viongozi wengine ambao wanakabiliwa na hatari ya kupoteza nafasi zao kutokana na “ndoa” kati ya Rais Ruto na Odinga ni Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Maspika Moses Wetang’ula (Bunge la Kitaifa) na Amason Kingi (Seneti).

Katika kambi ya Bw Odinga, wale ambao huenda wakapoteza ni viongozi wanaopinga serikali jumuishi wakiongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna.

Wengine katika kundi hili, na ambao wamebuni vuguvugu la Kenya Moja, ni wabunge Babu Owino (Embakasi Mashariki), Caleb Amisi (Saboti), Antony Kibagendi (Kitutu Chache Kusini), miongoni mwa wengine.